Na John Walter-Manyara

Mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere  Desemba 7,2021 amezindua Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya mkoa na kuwasisitiza kuendelelea kujikinga dhidi ya Uviko-19 kwa kupata Chanjo na kuhamasisha wengine kufanya hivyo.

Nyerere ameagiza Halmashauri zote za mkoa wa huo ambazo bado hazijaunda mabaraza ya wafanyakazi, kufanya hivyo mara moja.

Amewasihi watumishi kufanya kazi kwa weledi,kutunza siri za serikali na kutofanya kazi kwa mazoea ili kuongeza tija kazini,lakini pia kuepuka majungu kazini.

Amewataka wajumbe wa baraza hilo kuwa chachu kwa wafanyakazi waliowatuma katika baraza na kutumia nafasi hiyo katika vikao vya baraza kuweza kuishauri vyema menejimenti katika kutatua changamoto mbalimbali za wafanyakazi.

Amelitaka Baraza hilo litumike ipasavyo kujadili malengo ya serikali pamoja na maslahi ya watumishi, na mtu yeyote akiona kuna tatizo apeleke kwenye Baraza la Wafanyakazi kwani  ndio sehemu sahihi ya kutatua changamoto zao.

 Pia amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kuhakikisha wanasimamia vyema yale yote ambayo wafanyakazi wanapaswa kuyafanya kwenye maeneo yao ya kazi.

Aidha amewapongeza Katibu aliyechaguliwa  Ndugu Emanuel Bura na Katibu msaidizi Zulfa Laizer ambao  wataongoza Baraza hilo lenye wajumbe 46  kwa kipindi cha Miaka mitatu.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi mwenyekiti wa TUGHE mkoa wa Manyara Nobert Kyomushula amesema wamepokea maelekezo ya mkuu wa mkoa na wapo tayari kuyafanyia kazi maagizo hayo ikiwemo kushiriki katika mapambano dhidi ya Uviko-19.

Amesema watahakikisha wao kama wafanyakazi wanatimza wajibu wao kabla ya kudai haki.
Kyomushula  alimuomba mkuu wa mkoa kuwa mlezi katika baraza hilo,ombi ambalo mkuu wa mkoa Makongoro Nyerere amelikubali.

Baraza la Wafanyakazi sekretarieti ya mkoa wa Manyara litakuwa na majukumu ya kuwashirikisha wafanyakazi wa serikali katika utekelezaji wa shughuli kwa ushirikiano na uongozi, kuishauri serikali juu ya ufanisi  wa kazi na hatua zinazofaa kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa huduma zitolewazo na wafanyakazi wa serikali kwa taifa ni za kuridhisha na zimo katika lengo la taifa la kuleta maendeleo ya nchi.

Aidha majukumu mengine ni kushauri serikali juu ya mambo mengine muhimu yanayohusu maslahi na hali bora za wafanyakazi wa serikali, kushauri juu ya utaratibu wa kupandishwa vyeo na nidhamu serikalini na kushauri masuala ya Afya kwa watumishi hususani Ukimwi sehemu za kazi.

Majukumu mengine ya baraza hilo ni Kushauri juu ya Muundo wa utumishi serikalini, kupokea na kuthibitisha mipango ya makisio ya mapato na matumizi ya sekretarieti, Kujadili na kutoa ushauri kuhusu mipango ya Elimu kwa wafanyakazi kwa ujumla na Elimu ya ujuzi, kujadili na kutoa ushauri katika matumizi ya fedha kufuatilia na Kasma pamoja na kujadili na kushauri taratibu za vivutio.
Share To:

Post A Comment: