Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Amos Maganga (kushoto), akizungumza na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ilambabusungu, Kijiji cha Bubiki, Wilaya ya Kishapu, Mkoani Shinyanga, Mwandu Fimbo (kulia) wakati wa ziara ya Bodi ya Nishati Vijijini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme, Septemba 7 mwaka huu. Wa pili – kulia ni Mjumbe wa Bodi, Oswald Urassa.

Veronica Simba – Shinyanga

Serikali imewashukuru Wabia mbalimbali wa Maendeleo kutokana na mchango wanaoendelea kutoa katika kuwezesha utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Amos Maganga alitoa shukrani hizo Septemba 7 mwaka huu wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mkoani Shinyanga.

Akishiriki katika ziara ya Bodi ya Nishati Vijijini (REB) kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, hususan mradi wa ujazilizi mkoani humo, Mhandisi Maganga alibainisha kuwa Wabia hao wa Maendeleo wana mchango mkubwa katika kufanikisha mradi husika.

Aliwataja Wabia hao kuwa ni Serikali za Norway, Sweden pamoja na Umoja wa Ulaya ambao kwa umoja wao wamefadhili shilingi bilioni 147 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili A katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Kilimanjaro na Tanga.

“Wamekuwa nasi bega kwa bega kuhakikisha kwamba azma ya Serikali kuwapatia wananchi huduma mbalimbali ikiwemo nishati ya umeme inafikiwa hivyo kupunguza hali ya umaskini katika maeneo husika,” alisema.

Mhandisi Maganga aliongeza kuwa, wajibu wa REA ni kuhakikisha msaada uliotolewa unatumika kama ilivyokusudiwa na Wabia hao wa Maendeleo ili malengo yaliyodhamiriwa yaweze kufikiwa.

Aidha, alitumia jukwaa hilo kuwakaribisha kutembelea miradi waliyoifadhili katika maeneo mbalimbali nchini ili wajionee maendeleo ya utekelezaji wake.

Bodi inaendelea na ziara katika Mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa kupitia REA. 

Share To:

Post A Comment: