Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila na kamati ya Usalama wilaya wamefanya ukaguzi wa barabara ya Ngenge -Kaiho yenye urefu wa km 10, ujenzi wa kuwango cha zege barabara ya Rushwa-Kishuro mita 200, ujenzi wa barabara ya Ngenge - Kishuro Km 2 na ujenzi wa kalvat 4 na ukarabati wa mitaro ya Nshamba mjini.


Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mhe. Toba Nguvila amepongeza ujenzi wa kiwango cha zege katika barabara ya Kishuro uliokidhi viwango na haja za wananchi kwani imewasaidia wananchi wa Kata ya Ngenge àkupitisha magari yao kwenye barabara bila shida na kuepusha ajali hususani kwenye eneo hilo korofi.


"Tumeridhika na utekelezaji wa ujenzi wa barabara hizi, zimejengwa kwa kiwango ambacho kinakidhi haja za wananchi wetu. Kwa kujenga hii barabara ya Rushwa-Kishuro kwa kiwango cha zege inawasaidia sana wananchi  kwa sababu vyombo vya moto na magari yanapita kwa uhakika bila kuteleza wala kuanguka. Kwa niaba ya wananchi wa Muleba tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizi", ameeleza Mhe. Toba Nguvila.


Pamoja na utekelezaji mzuri Mhe. Nguvila amewaagiza TARURA kufanya maboresho hasa kwenye maeneo ambayo ni korofi kwa kuweka mitaro ya maji pamoja na makalavati ya kupitisha maji kwani  pasipo kuweka mitaro kwa ajili ya kupitisha maji barabara zitaharibika mapema na hazitadumu kwa muda mrefu.


Wananchi pamoja na waendesha vyombo vya moto wanaotumia barabara hiyo wameishukuru Serikali pamoja na uongozi wa Wilaya kwa kuona umuhimu wa kuwaboreshea barabara hiyo kwa kiwango cha zege eneo la mita mbili ambalo lilikuwa sio salama kupitika kwani baada ya ujenzi wa barabara hiyo imewasaidia kupita kwa urahisi, kusafirisha bidhaa mbalimbali kutoka ndani ya kata yao na hata kusaidia kuongeza pato la kijiji.


Barabara ya Ngenge-Kishuro km 2 pamoja na ujenzi wa kalvati 4 umegharimu Tsh. 38,378,568.76, barabara ya Ngenge-Kaiho km 10 umegharimu Tsh. 67,011,798.52 na ujenzi wa kiwango cha zege barabara ya Rushwa-Kishuro m 200 umegharimu Tsh. 57,742,434.34


Imetolewa na:


Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,

Halmashauri ya wilaya ya Muleba.

Share To:

Post A Comment: