Jane Edward, Arusha


Aliyekuwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali(CAG), Ludovick Utouh, amesema bado kuna tatizo kubwa kwa viongozi wakuu wa mashirika ya umma na taasisi binafsi kuwaingilia Wakaguzi wa Ndani katika utekelezaji wa majukumu yao.


 Mkaguzi huyo wa zamani na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali, alisema kuingiliwa kwa Wakaguzi wa Ndani katika majukumu yao kuna punguza ufanisi na utendaji kazi kwa kuwa hawapo huru kuwajibika ipasavyo.


Utouh,aliyasema hayo  jijini Arusha wakati, akitoa mada katika mkutano wa Wakaguzi wa ndani wa Tanzania na baadhi ya wakaguzi kutoka  mbalimbali za Afrika, pamoja na Wakuu wa taasisi za umma na binafsi, uliondaliwa na Tasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania(IIA).


Mkutano huo, umewakutanisha wajumbe zaidi ya 300,kuelekea mkutano wa nane wa taasisi hiyo utakaofunguliwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba, Septemba 22 mwaka huu.


Alisema awali wakaguzi wa ndali walipaza sauti kulalamikia kuingiliwa katika majukumu yao na viongozi wao wakuu katika mashirika na taasisi zao.


“Hali ya sasa siwezi kusema kwamba imetengemaa bado kwa sababu kama mtakumbuka CAG, alipotoa ripoti yake Aprili mwaka huu,kuna halmashauri zilipata hati chafu na likatoka tamko la kuchukuliwa hatua kwa wakaguzi wa ndani.


“Kwa sisi tunavyofahamu namna wakaguzi wa ndani wanavyofanya kazi tulisema tamko lile lilikuwa la bahati mbaya sana kwa kuwa wakaguzi wa ndani wao wanashauri na hawana mamlaka ya kutekeleza yale wanayoelekezwa kwa hiyo watu wakuchukuliwa hatua kwa kupatikana kwa hati chafu ni maofisa masuhuli ambao ndio wana wajibu wa kutekeleza mapendekezo yanayotoka katika ukaguzi wa ndani.alisema”


Katika hatua nyingine alisema kuna umuhimu wa uwajibikaji katika mpango wa kuleta maendeleo kwa kuwa maendeleo duniani yanakwenda sambamba na uwajibikaji.


“Nilitoa mada inayohusu uhusiano wa uwajibikaji na maendeleo niliangalia zaidi kwenye taaluma ya ukaguzi wa ndani na wanahusikaje kwa sababu nchi inalilia sana maendeleo na Watanzania wanataka kupata maendeleo, mkutano huu umelenga kukumbushana na kuelimishana kwa kuangalia uwajibikaji ni kitu gani na maendeleo ni nini na vitu hivyo vina mahusiano pamoja na nafasi ya wakaguzi wa ndani katika kuleta maendaleo,”.


Mratibu wa mkutano huo,Zelia Njeza, alisema lengo la mkutano huo ni kutoa elimu kwa wakuu wa taasisi za umma na mashirika pamoja na wajumbe wa bodi.


Alisema katika mkutano huo wamezungumzia suala la uwajibikaji na utawala bora kwa  mashirika na taasisi hizo kwa kuwa wanapotekeleza  majukumu yao wahakikishe shughuli hizo zinafanywa kwa maslai ya taasisi hizo na Taifa kwa ujumla.


“Tunaweza kutoa elimu kwa hawa Wakurugenzi wa mabodi mbalimbali hapa nchini kwa ajili ya kuwawezesha wanapokuwa wakitoa huduma yao kuhakikisha taasisi zinajiendesha vizuri kwa malengo yao nan chi kwa ujumla kufahamu ni vitu gani wanavyotakiwa kuviandaa.


“Sisi kama wakaguzi pia tutajikita zaidi kuhakikisha tunazingatia suala la utawala bora na uwajibikaji katika kazi na kutoa ushauri katika Nyanja mbalimbali ikiwamo utawala bora,vihatarishi katika utendaji na namna ya kuthibiti.alisema Njeza”


Aidha alisema bila ya kuwa na utawala bora hakutakuwa na maendeleo na taasisi na nchi hazitaweza kujiendesha kwa kuwa huo ndio moyo na chachu ya kuleta maendeleo katika jamii.


Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Biashara ya Dar es Salaam (DCB), Zawadi Nanyaro, alisema kupitia mkutano huo wamejifunza kusimamia kampuni,taasisi na mashirika na namna ya kukabiliana na viashiria vinavyoweza kujitokeza kazini ikawamo kupata hasara na wizi unaoweza kujitokeza.


“Awali wakaguzi tulikuwa tunaingiliwa katika majukumu yetu na viongozi kwa kutokujua madhara yake kwa kuwa kiongozi kazi yake ni kutoa maamuzi na wakaguzi wanatakiwa kufanya shughuli zao wakiwa na uhuru ili kutoa taarifa sahihi zinazohitajika,”alisema Zawadi.

Share To:

Post A Comment: