Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendeleza zao la zabibu na kuhakikisha linaleta tija kwa wakulima.

“Serikali imeanzisha kampeni ya kuhamasisha kilimo cha zao la zabibu, tunataka kumsaidia mkulima kuanzia maandalizi ya shamba, upatikanaji wa pembejeo hadi hatua ya mauzo.”

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Julai 5, 2021) alipotembelea Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania katika eneo la uzalishaji miche ya zabibu, mashamba na viwanda vya zabibu, Dodoma.

Pia, Waziri Mkuu ametembelea kiwanda kidogo cha kuchakata zabibu kilichopo eneo la Msalato, jijini Dodoma kinachimilikiwa na mkulima mdogo Bw. Phortunatus Kenyunko.

Mbali na kutembelea kiwanda hicho kidogo, pia Waziri Mkuu ametembelea kiwanda kikubwa cha kutengeneza mvinyo wa zabibu cha Cetawico kiilichopo Hombolo, jijini Dodoma.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wakulima wa zabibu kwamba Serikali imedhamiria kuboresha kilimo cha zao hilo kwa sababu kilimo ni mkombozi kwa Watanzania.

Amesema kampeni hiyo itaanzia mkoa wa Dodoma kwa kuwa imegundua kwamba zabibu ni fursa ya kiuchumi nchini na ardhi yote ya wilaya za mkoa wa Dodoma inakubali kilimo hicho.

Katika kuhakikisha kilimo hicho kinapata mafanikio, Waziri Mkuu amezitaka taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ibadilike na kutoa mikopo kwa wakati.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametembelea skimu ya umwagiliaji ya mashamba ya wakulima wa zabibu iliyopo Hombolo na amewasisitiza wakulima walinde miundombinu hiyo.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: