Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy
Gwajima akizungumza na wandishi wa habari katika Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Dodoma wakati alipokutana na Viongozi wa Mkoa wa Dodoma na
kusisitiza kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari ya Corona.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka akitoa maelekezo kwa Viongozi wa Mkoa wa Dodoma na Wilaya zake kuhusu kuchukua tahadhari za ugonjwa wa COVID-19.
Charles James,
SERIKALI
imewataka viongozi ngazi ya Mikoa na Wilaya Nchini kuhakikisha kwamba
wanahamasisha wananchi kuchukua tahadhari na hatua zote za kujikinga na
ugonjwa wa COVID-19 'Corona'.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini
Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Dk Dorothy Gwajima wakati alipokutana na viongozi wa Mkoa wa Dodoma na
Jiji la Dodoma na kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Waziri
Gwajima pia amekiri kwamba katika wimbi la kwanza na la pili la ugonjwa
wa Corona bidhaa za tiba asili zilisaidia katika mapambano dhidi ya
ugonjwa huo huku akisisitiza kwamba hawajazifuta.
" Niwaombe
viongozi wa mikoa yote nchi kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi juu
ya kuchukua tahadhari na hatua za kujikinga, maeneo yenye mikusanyiko
kuwepo na watoa elimu.
Wananchi wavae barakoa, wawe na vitakasa
mikono na kuwepo na maji tiririka kwenye maeneo yote yenye mkusanyiko,
daladala pia watu wakae level siti na maeneo ya masokoni na makanisani
kuwepo na maji tiririka na uvaaji barakoa," Amesema Waziri Gwajima.
Amesema
watanzania tayari walishakutana na wimbi la kwanza na lile la pili
hivyo wanapaswa kutumia uzoefu walioupata kwenye wimbi lililopita katika
kuishi na wimbi la tatu kwa kufuata tahadhari zinazotolewa na wataalamu
wa afya.
" Kama wimbi la kwanza na la pili tuliishi nalo basi
hata hili la tatu tunaweza kuishi nalo kiuzoefu. Bidhaa za Tiba asili
hatujazifuta na tunakiri hatutozifuta na hatutoziacha ni wazi
zilitusaidia sana," Amesema Dk Gwajima.
Amesema kama ambavyo Rais
Samia alisema ni kweli Tanzania tayari ina wagonjwa kadhaa wenye
ugonjwa huo hivyo ni vema kila mmoja kuchukua tahadhari za kujilinda
yeye na mwenzake.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony
Mtaka ametoa maagizo kwa Mkuu wa Kikosi cha Barabarani mkoani humo
kuhakikisha maagizo ya daladala kupakia abiria level siti na ambaye
atakaidi agizo hilo achukuliwe hatua.
RC Mtaka ameagiza pia
mameneja wa masoko yote ya Mkoa wa Dodoma kuhakikisha maji tiririka
yanakuepo kwenye masoko yao pamoja na kila mfanyabiashara kuvaa barakoa.
"
Niwaombe wananchi wote kujilinda na kulinda wenzake, tukumbuke anakufa
ni nafsi siyo Serikali hivyo tuchukue tahadhari, tuvae barakoa, tuepuke
mikusanyiko isiyo na lazima na tunapotoka basi tubebe vitakasa mikono,
tupunguze pia kugusana na kukumbatiana.
Kwenye maeneo ya biashara
pia hatua zote za kujikinga zichukuliwe, na kwenye nyumba za ibada
tuepuke kushikana mikono na vifaa vya kujikinga viwepo," Amesema RC
Mtaka.
Post A Comment: