Na Andrew Chale, Zanzibar. 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dokta. Hussein Ali Hassan Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio za Kimataifa za Zanzibar zijulikanazo kama Zanzibar International Marathon zinazotarajiwa kukimbiwa 18 Julai, mwaka huu mjini Unguja zenye lengo la kukuza uchumi wa bluu.

Waratibu wa mbio hizo wamesema hayo wakati wa utambulisho rasmi kwa wadau na Wanahabari  ambapo walieleza kuwa, lengo la mashindano hayo ni kukuza na kuchochea Utalii visiwani humo.

"Lengo la mashindano haya ni kukuza na kuchochea Utalii visiwani Zanzibar baada ya mtikisiko wa janga la CORONA lililoikumba Ulimwengu mwishoni mwa mwaka 2019." Alisema Msemaji wa mbio hizo, Hassan Mssa Ibrahim.

Aidha, alibainisha kuwa, Washiriki wa Marathon hiyo ni watalii wa ndani na nje, Taasisi, Wanafunzi wa Vyuo vikuu na wananchi kwa ujumla na yatakuwa endelevu kila mwaka.

"Tunawaomba Wadau waendelee kutupokea na kujitokeza kwa wingi katika kutuunga mkono. lengo la mashindano haya ni kukuza na kuchochea Utalii wetu hapa visiwani.

Katika siku hiyo ya mbio 18 Julai, kutakuwa na mbio za kuanzia Kilometa: KM 5, KM10, KM 21na pia kutakuwa na mbio maalum za Watoto za Mita: M 700 huku bingwa wa Marathon akitarajiwa kupata zawadi, Pia Washiriki wote watapewa zawadi maalum ya Zanzibar kutoka kwa mgeni rasmi". Alisema Hassan Mussa Ibrahim.

Aliongeza kuwa, Katika mbio hizo, zenye kauli mbiu; "Tunakuza uchumi wa bluu kupitia michezo Zanzibar", ambapo sehemu ya mapato yatakayopatikana yanatarajiwa kwenda kituo cha kuwatunza Wazee Sebleni.

Aidha, Hassan Mussa Ibrahim  alisema washiriki watalipia Tsh. 35000,  kwa Watanzania na Wakazi wa Afrika Mashariki, kwa wageni wa nje watalipia dola USD 50 na Tsh 20000 kwa Wanafunzi wa Vyuo huku kwa watoto watalipia 15000.

"Tayari vituo mbalimbali unaweza kufanya malipo kwa Dar es Salaam ni maduka ya Dauda sports,Maduka ya Just Fit sports gear Kijitonyama na Mlimani cty.

Kwa upande wa Zanzibar watalipia kupata ushiriki kupitia CATALUNIA barbershop,  Park Hyatt Zanzibar, Cape Town fish market Zanzibar na sehemu nyengine zitatangazwa na taratibu zingine kupitia tovuti maalum ya mashindano". Alimalizia Hassan Mussa Ibrahim.

Katika utambulisho huo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mhe. Lelant Mussa pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo: Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini, Mhe. Ayou, Mkuu wa Wilaya ya Mjini Mhe. Rashid Msaraka, katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, vijana na michezo, Kamishna wa Michezo Zanzibar na Wakuu wa Taasisi mbalimbali pia Wadau, wadhamini pamoja na Mabalozi wa mbio hizo, Zembwela na Maulid Kitenge.

Share To:

Lucas Myovela

Post A Comment: