Mkuu wa Wilaya Bunda mkoani Mara, Mwl. Lydia Bupilipili amelipongeza shirika la KIVULINI kwa uratibu mzuri wa shughuli zake za kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia wilayani humo.


Mwl. Bupilipili ametoa pongezi hizo Juni 04, 2021 kwenye hafla ya utoaji tuzo kwa wadau wa maendeleo wilayani Bunda iliyoandaliwa na Ofisi yake.


"Jamii ilikuwa haithamini mchango wa mwanamke, nilipokuja hapa siku moja nilizomewa kwenye mkutano, nilipoangalia nikakuta na wanawake wenzangu wanazomea kwamba siwezi kuongea wanaume wamekaa.  Lakini kupitia elimu tuliyotoa kwa kushirikiana na shirika la KIVULINI tumeondoa hali hiyo katika jamii" amesema Mwl. Bupilipili na kuongeza; 


"Kulikuwa na matukio mengi ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake hususani vipigo, tuliendelea kutoa elimu na kuchukua hatua za kisheria na sasa matukio hayo yamepungua na tutahakikisha tunayatokomeza" amesisitiza Mwl. Bupilipili.


Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda imetambua mchango wa wadau wote wa maendeleo wilayani humo kwa jitihada zao za kushirikiana na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya elimu, afya na maji.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: