Kaimu Katibu tawala wa Mkoa wa Mbeya Bi. Mwajabu Nyamkomora akifungua semina ya umuhimu wa vipimo katika sekta ya afya iliyofanyika katika ukumbi wa Dr. Shein jijini Mbeya mapema leo. Nyamkomora alitoa wito kwa watoa huduma za afya,madaktari,wauguzi na watu wa maabara kulinda afya za Watanzania kwa kuzingatia upimaji sahihi, kufuata miongozo pamoja na viwango vya kitaifa na kimataifa .

Mkuu wa Maabara ya Ugezi Bw.James Mahilla akizungumza na washiriki wa semina ya umuhimu wa vipimo katika sekta ya afya iliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Shein jijini Mbeya. Mahilla alisema ili kuenzi siku ya vipimo duniani,TBS imeandaa semina kwa lengo la kutoa uelewa kwenye masuala ya sayansi ya Vipimo hususani katika sekta ya Afya

Meneja wa Kanda Nyanda za juu kusini Bw.Abel Mwakasonda akizungumza na washiriki wa semina ya Umuhimu wa Vipimo katika sekta ya afya iliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Shein Jijini Mbeya mapema leo. Mwakasonda alisema TBS kwa kushirikiana na taasisi zingine zenye dhamana ya kushughulika na vipimo zimejipanga kuhakikisha kila mtoa huduma katika sekta ya afya anapata uwezo wa kutoa huduma kwa kuzingatia vipimo sahihi.

Washiriki wakiwa katika semina ya Umuhimu wa Vipimo katika sekta ya afya iliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Shein Jijini Mbeya mapema leo.


Watoa huduma katika sekta ya afya na wadau wote kila mmoja kwa nafasi yake wametakiwa kuchukua hatua stahiki kwa pamoja kuhakikisha wanalinda afya za Watanzania kwa kuzingatia upimaji sahihi, kufuata miongozo na viwango vya kitaifa na kimataifa.

Wito huo umetolewa leo Mei 27 2021 na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mwajabu Nyamkomora, katika semina iliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa lengo la kutoa uelewa kwenye masuala ya Sayansi ya Vipimo hususani katika sekta ya afya kwa wadau.

Semina hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani yaliyofanyika Mei 20, mwaka huu kitaifa mkoani Dodoma, kauli mbiu ikiwa na ujumbe usemao; "Umuhimu wa Vipimo Katika Sekta ya Afya."

Nyamkomora alisema vipimo ni huduma muhimu sana katika utoaji wa huduma za afya na uzalishaji wa dawa katika viwanda vyetu, kwani Taifa ambalo watu wake hawana afya, haliwezi kuzalisha.

Aliongeza pia ni muhimu watoa huduma za afya, madaktari, wauguzi na watu wa maabara, watoe huduma kwa kuzingatia viwango, miongozo ya Serikali, weledi, kujituma na kufanya kazi kwa bidii na kwa kukumbuka viapo vyao.

"Lakini pia tutambue kuwa uhai na ustawi wa taifa letu upo katika mikono yenu (watumishi wa afya) hivyo wafanye kazi kwa bidii," alisema, Nyamkomora.

Mgeni huyo rasmi, Nyamkomora aliwataka watoa huduma katika sekta ya afya kujitathmini kama wanatoa huduma ya vipimo inayokidhi viwango.

"Tujikague kwa kujiuliza maswali. Je, una elimu, ujuzi na maarifa ya kutosha kutumia vifaa unavyotumia katika upimaji, je, hali ya vifaa unavyovitumia inaruhusu kufanya vipimo? Je, tunafuata ushauri wa kitaalamu kuhusu matumizi, utunzaji, matengenzo ya muda na yale ya baada ya hitilafu kwa vifaa tunavyotumia?" Alihoji, Nyamkomora na kuongeza;

"Mtoa huduma anatakiwa kujiuliza kama kifaa chako kimehakikiwa kwa usahihi wake wa kutoa majibu sahihi? Je, umefanya ugezi (Calibration) kwenye vifaa vyako?

Unatumia cheti cha ugezi kutoka kwa aliyekupa huduma hiyo? je,aliyekupa huduma ya ugezi ana weledi wa kazi anayofanya na je mfumo wa kuhakiki majibu yanayotoka ni sahihi?"

Alisema ni muhimu kila mmoja kwa nafasi yake akachukua hatua stahiki ili wote kwa pamoja tuhakikishe wanalinda afya za Watanzania kwa kuzingatia upimaji sahihi, kufuata miongozo na viwango vya kitaifa na kimataifa.

Alisema ni matumaini yake kuwa baada ya semina hiyo kila mmoja kwa nafasi yake atachukua hatua stahiki ili wote kwa pamoja tuhakikishe tunalinda afya za Watanzania.

Kwa upande wa Meneja wa TBS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Abel Mwakasonda, alisema vifaa vinavyotumika katika uchunguzi wa afya vina mchango mkubwa katika kuhakikisha ugonjwa ambao mtu anaugua.

Aliwataka wamiliki na waendeshaji wa hospitali, maabara za afya, viwanda vya kuzalisha dawa na taasisi zinazosimamia sekta ya afya kutambua kuwa huduma bora za afya zinawezekana tukizingatia ubora wa vipimo vyetu.

Alisema mtoa huduma katika sekta ya afya anapata uwezo wa kutoa huduma kwa kuzingatia vipimo sahihi.

"Vipimo sahihi ni huduma muhimu sana katika utoaji wa huduma bora za afya, nawashauri wamiliki wa viwanda, hospitali, vituo vya afya, maabara za uchunguzi na watoa huduma wote wa sekta ya afya mtumie vipimo sahihi kwa wakati sahihi na kupata huduma ya ugezi wa vifaa (mashine zinazotumika kupimia ama kutunzia sampuli zenu kutoka katika Taasisi zinazofanya vipimo kwa usahihi ili muweze kutoa huduma bora kwa Watanzania," alisema Mwakasonda na kuongeza;

"Vipimo sahihi ni kiwezeshi cha utoaji wa huduma bora na salama. IIi kuenzi siku ya Vipimo Duniani."

Kwa upande wa Mkuu wa maabara ya ugezi Bw.James Mahilla alisema TBS kupitia Maabara ya Vipimo (Metrolojia) ndiyo watunzaji wa Viwango vya Taifa vya Vipimo.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: