Afisa Maliasili  katika halmashauri ya Itigi, John Makotta akijibu hoja mbalimbali  zilizotolewa na Madiwani wa Baraza hilo kuhusiana na tembo waharibifu pamoja na simba. Madiwani wa Halmashauri ya Itigi mkoani Singida wakiwa kwenye kikao cha Baraza hivi karibuni.


 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Itigi, Mhe. Hussein Simba akifungua KIkao cha Baraza la Madiwani hivi karibuni

 


Na Abby Nkungu, Itigi


WAKULIMA katika halmashauri ya Itigi Mkoani Singida wameshauriwa kupanda pilipili na kutundika mizinga ya nyuki kuzunguka mashamba yao kama njia mojawapo ya kudhibiti tembo wanaoshambulia mazao ya chakula na kuleta uharibifu mkubwa hali inayoweza kusababisha janga la njaa. 

Mwito  huo  ulitolewa na Ofisa Ardhi na Maliasili katika halmashauri hiyo, John Makotta  wakati akijibu hoja za madiwani kwenye kikao cha Baraza, waliolalamika kuwa mashamba  mengi ya wakulima katika kata zao huvamiwa na tembo kiasi cha kusababisha uharibifu mkubwa wa mazao.

Katika  hoja yake Diwani wa kata ya Kitaraka,  John Subeti alisema licha ya  kutoa taarifa kwa idara husika kila mara tembo wanapoingia kwenye mashamba, hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa kuwadhibiti na kwamba bado wanaendelea kuharibu mazao ya chakula na biashara hali inayoweza kuleta athari  kubwa kiuchumi. 

Naye Diwani wa kata ya Ipande, Kedimon Mpondo  alisema  kuwa yapo madhara makubwa  yanayojitokeza kwenye kata zilipo jirani na maeneo ya  hifadhi  kutokana na uharibifu wa mazao unaosababishwa na tembo na mifugo kuliwa na simba.

Madiwani hao waliungwa mkono na wenzao kutoka  kata  mbalimbali wakiomba Mamlaka husika  kwenda  haraka  maeneo yenye wanyama hao kuwaondoa ili  kuwanusuru wananchi kukumbwa na janga la njaa. 

Akijibu hoja hizo, Makotta alikiri kuwa  upo mfumko wa wanyapori wengi  wanaovamia mashamba ya watu  na  amekuwa akijitahidi  kuomba msaada wa askari mara kwa mara  kutoka  kwenye Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya  Kati  (KDU) kwa ajili ya kwenda kuwafukuza. 

"Idara yangu inakabiliwa na changamoto ya upungufu mkubwa wa watumishi ambapo kwa hivi sasa nipo peke yangu pia, kuna uhaba wa vitendea kazi. Lakini, kwa kusaidiana na maaskari wa KDU huwa najitahidi kufika kwenye kila tukio mara ninapojulishwa" alisema Makotta na kuongeza; 

Simba ni rahisi kuwahamisha kwa gari na kuwapeleka maeneo mengine lakini si rahisi kuhamisha tembo. Ili kuwadhibiti tembo kufika kwenye mashamba yenu, nashauri wakulima walime pilipili kando kando ya mashamba au kutundika mizinga ya nyuki. Mbinu hii inasaidia sana kuwazuia tembo kufikia mashamba".

Alisema njia nyingine ya kudhibiti wanyama wote waharibifu ni kuwaua kwa risasi au kwa njia nyingine yoyote lakini akatahadharisha kuwa ni lazima taarifa itolewe kwenye idara ya Maliasili kila anapouawa tembo au simba.                                        


"Hakikisheni kila anapouawa mnyama nyara zote za Serikali kama meno na mkia kwa upande wa tembo na ngozi na kucha kwa upande wa Simba zinaondolewa na kukabidhiwa idara ya Maliasili" alisema na kusisitiza kuwa wananchi wasigawane nyama ya mnyama anayeuawa bila ruhusa kutoka Maliasili.

Share To:

Post A Comment: