Na Elizabeth Joseph,Arusha.


Mkuu wa Wilaya ya Arusha Kenani Kihongosi amekemea kitendo cha baadhi ya watu wanaojiita ni Waandishi wa Umma kwa kusema kazi hiyo ni utapeli kwa wananchi hivyo kuwataka waache mara moja.


Aliyasema hayo jana wakati akiongea na wananchi wa Kata mbalimbali katika ziara aliyoifanya eneo la kwa Mrombo kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi.


Alisema kuwa waandishi hao Umma wamekuwa wakiandikisha mikataba mbalimbali hasa ya uuzaji na ununuzi wa viwanja jambo alilosema ni utapeli kwakuwa mikataba hiyo huandikwa kwa mujibu wa sheria na sio kiholela."Waandishi wa Umma katika maeneo ya serikali wasifanye kazi wa wananchi na wananchi tulishawaambia hili jambo sasa wale wanaokubali kutapeliwa hiyo inakuwa msalaba wao wenyewe, jukumu lao wananchi ni kufuata maagizo tunayotoa ili wasiingie kwenye migogoro isiyo ya lazima"aliongeza Mkuu huyo.


Aidha alieleza kuwa endapo mtu anataka kuuza ama kununua eneo ni vizuri kuwatafuta Wenyeviti wa Mtaa au Kijiji,Watendaji ama Maosifa Tarafa wa maeneo yao pamoja na mwanasheria ili aandikishe mikataba kwa kufuata sheria za nchi.


Katika ziara hiyo Kihongosi aliongozana na Watendaji wa Idara mbalimbali ikiwemo TARURA,Idara ya Maji,OCD, TANESCO na Idara nyingine ambapo malalamiko mengi ya wananchi yalikuwa ni ucheleweshaji wa kuunganishiwa  maji,umeme pamoja na migogoro ya ardhi inayosababishwa na waandishi wa Umma.


Mwisho.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: