Nteghenjwa Hosseah, Bahi


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi.


Waziri Ummy ameonyesha hali hiyo wakati wa ziara yake Wilayani humo kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na kamati ya fedha pamoja na menejimenti.


Hapo awali Waziri Ummy alifanya ziara katoka Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ambapo hakuridhishwa na usimamizi wa miradi ya maendeleo halikadhalika upelekaji wa asilimia 40 ya mapato ya ndani katika miradi ya maendeleo.


Pia akiwa Chemba  hakuridhishwa na matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo kwa kuwa ilionekana fedha hizo kutumika kwa ajili ya posho za safari na vikao.


Katika Wilaya ya Bahi ziara  ya Mhe Ummy ilianzia katika shule ya Sekondari Mundemu ambapo alikagua ujenzi wa bweni na madarasa yaliyojengwa kwa kutumia fedha za mradi wa Lipa Kulingana Matokeo (EP4R).


Akiwa shuleni hapo, Mhe Ummy alionyesha kuridhishwa na usimamizi wa fedha za miradi hiyo kwani thamani ya fedha inaonekana.


“Bahi mmepokea shilingi milioni 128 na mmefanikiwa kujenga bweni, madarasa mawili na matundu ya vyoo na miradi yote imekamilika tena kwa ubora unaotakiwa hongereni sana viongozi wa Bahi” alisema Mhe. Ummy


" Kuna halmashauri zingine wameshindwa kukamilisha ujenzi wa bweni kwa milioni 80 sasa niwatake wote waje kujifunza Bahi namna bora ya usimamizi wa fedha za miradi ya maendeleo."


Katika hatua nyingine Mhe. Ummy ameridhishwa na upelekaji wa asilimia 40 ya fedha za mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo.


" Mpaka sasa Bahi mmekusanya zaidi ya shilingi milioni 900 na kwenye miradi mmepeleka shilingi milioni 380  hiki ndicho ninachotaka kukiona kwenye halmashauri zote, upelekaji wa fedha za miradi unapewa kipaumbele."


" Kizuri zaidi kwa Bahi ni kuwa fedha unaona zimeenda kwenye ujenzi wa zahanti, madarasa, mabweni yaani miradi ile halisi ya maendeleo na sio kulipana posho za safari na vikao fedha zimefanya kazi za maendeleo."


Mhe. Ummy aliongeza kuwa: " niwataka Halmashauri zote kuja kujifunza Bahi namna bora ya usimamizi wa fedha za miradi na upelekaji wa asilimia 40 ya mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo."


Wakati wa ziara hiyo, Mhe Ummy ameahidi kupeleka gari la wagonjwa kwa ajili ya kituo cha Afya cha Mundemu pamoja na Sh milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Mundemu.

Share To:

TANZANIA YA KIJANI

Post A Comment: