MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Asasi za Kiraia (NGOs) Mhe Neema Lugangira ameishauri Ofisi ya Waziri Mkuu kutoa mwelekezo wa mapambano dhidi ya udumavu na utapiamlo wa aina zote na kuzikaribisha rasmi Sekta ya Asasi za Kiraia kuandaa mpango kazi kwa kushirikiana nao kama ilivyofanya kwa Sekta Binafsi.

Alitoa ushauri huo Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia kwenye Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo Mh Neema Lugangira alijikita kwenye mambo mawili ya Lishe na Sekta ya Asasi za Kiraia (NGOs) kwa kutoa mchango wake.

Akizungumza wakati akichangia mambo hayo Mbunge Neema Lugangira aliipongeza Serikali kwa jitihada kubwa inayofanya kwa kuboresha hali ya lishe hapa nchini na kutokomeza udumavu na aina yoze utapiamlo.

“Napenda kupongeza jitihada kubwa zilizofanywa na Rais Samia Suluhu wakati akiwa Makamu wa Rais ambaye ilipelekea kumuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamiseni kusaini mikataba ya Lishe kwa niaba yake na Wakuu wa Mikoa. Hivyohivyo namshukuru sana Mhe Waziri Mkuu Kasim Majaliwa na Mhe Waziri Jenista Mhagama kwa namna ambayo wanavyoendelea kuratibu Masuala ya Lishe ambayo yanaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu” Alisema

Mbunge Neema Lugangira alisema wanafanya hivyo kwa kupitia maeneo manne ambayo ni (1) kusimamia utekelezaji wa mpango jumuishi wa Lishe wa Kitaifa; (2) kusimamia  vuguvugu la uongezeji kasi ya kuboresha hali ya lishe duniani; (3) kujuimisha jumbe la lishe kwenye jumbe Mbio za Mwenge wa Uhuru; na (4) katika kutekeleza vipaumbele vya lishe vilivyowekwa kwenye mpango wa maendeleo ya Taifa.

“Kipekee napenda kukishukuru Chama changu, Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa Chama pekee ambacho kimeweka kipaumbele kikubwa  kwenye lishe na mnaweza kurejea ukurasa wa 7,40,139 hadi 141 ambapo Chama hicho kimeweka malengo madhubuti ya namna gani itaekeleza serikali ya kuboresha hali ya lishe nchini na kutokomeza udumavu na aina zote za utapiamlo” Alisema

Hata hivyo Mbunge Neema Lugangira alisema hivi sasa Tanzania kuna changamoto kubwa sana ya Lishe Duni inayopelekea kutuweka kwenye hatari ya kutokuwa kizazi chenye nguvu kazi shindani kwa siku zijazo.

“Wengi tunaongelea ajira lakini ikiwa watoto wana lishe duni na wapo na udumavu hivyo nguvu kazi na kizazi cha kesho kitapatikana vipi ndio maana ya kuipa kipaumbele suala la Lishe hivyo nitumie fursa hii kuikumbusha Ofisi ya Waziri Mkuu itamke rasmi ina maoni gani kuhusu janga hilo la lishe bora” Alisema

Alienda mbali zaidi na kueleza kwamba pia Ofisi ya Waziri Mkuu itakwenda kufanya nini ili ihakikishe kwamba Sekta na Wizara zote zinakwenda kuhusika na suala hilo na wanakwenda kutekeleza yale yote yaliyoandikwa kwenye Ilani ya CCM.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: