Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akiwahutubia wanawake katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika jana wilayani humo, mkoani Singida. Kutoka kushoto ni Meneja wa Miradi wa TAHA, Elianchea Shang'a na  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi.

Meneja wa Miradi wa TAHA, Elianchea Shang'a, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akikabidhi zawadi kwa mshindi wa michezo, Mariam Rashid.
Zawadi ikitolewa kwa mshindi, Neema Martin.
Washindi wakionesha zawadi zao.
Wanawake wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo (wa pili kushoto waliokaa). Kutoka kushoto waliokaa ni Meneja wa Miradi wa TAHA, Elianchea Shang'a, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi na Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Aika Masawe.


Picha ya pamoja ya ishara ya upendo.
Mshindi wa mapishi Rehema Kulungu (kulia) akiwa na zawadi ya jiko baada ya kukabiddhiwa. Kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Aika Masawe.
Maadhimisho yakiendelea.
 

Na  Dotto Mwaibale,  Singida


WANAWAKE wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wametakiwa kutumia fursa walizonazo ili kuinuka kiuchumi. 

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo Edward Mpogolo wakati akiwahutubia wanawake hao katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika juzi wilayani humo. 

Wanawake  hao wamepatiwa mafunzo ya kilimo cha mboga mboga na  matunda na Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA. 

" Wilaya yetu ya Ikungi ina fursa mama zangu tuzitumie ..sisi tuna fursa ya kuuza kuku Dodoma ambako wananunua kwa sh.15, 000 wakati sisi tunanunua kuanzia sh.9, 000, 8,000, 7, 000 hadi 5,000." alisema Mpogolo. 

Mpogolo aliwataka  wanawake hao kujiunga katika makundi ili waweze kuanzisha ufugaji wa mbuzi ambao soko lake lipo Dodoma na Arusha ambako kuna kiwanda na uwezo wake ni asilimia 100 lakini kinapata mbuzi asilimia 50 hadi 40 tu. 

Katika hatua nyingine aliwapongeza wanawake hao kwa kuwa waaminifu kwa kurejesha mikopo wanayokopeshwa na halmashauri ukilinganisha na wanaume ambao wanachangamoto ya urejeshaji. 

Aidha Mpogolo amewataka wanawake hao kuacha kujiingiza kukopa mikopo umiza yenye riba kubwa ambayo inawarudisha nyuma kiuchumi. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi alisema wilaya hiyo inatekeleza agizo la Serikali la kuwawezesha wanawake kiuchumi na akatumia nafasi hiyo kuipongeza Asasi ya TAHA na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN WOMEN) kwa kutoa mafunzo hayo na akaahidi kushirikiana nao. 

Meneja wa Miradi wa TAHA, Elianchea Shang'a alisema kwa kuwa mradi huo wanaoshirikiana na UN WOMEN pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi unaohusu kuwakomboa wanawake kiuchumi kupitia kilimo cha mboga mboga na matunda na unatekelezwa katika Wilaya mbili moja, Ikungi-Singida na  Msalala-Shinyanga. 

Alisema asasi hiyo yenye makao makuu yake jijini Arusha imejikita zaidi kuwawezesha wadau katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mboga mboga, matunda, maua, viungo na mazao ya mizizi. 

Katika maadhimisho hayo wilayani humo asasi hiyo ilitoa mafunzo ya ujasiriamali na utawala wa fedha pamoja na lishe ambapo washindi walipewa  zawadi mbalimbali.

Share To:

Post A Comment: