Na Dotto Mwaibale, Singida
VIJANA mkoani hapa wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais Dkt. John Magufuli kilichotokea Jana.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa jana kwa niaba ya vijana hao Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida Frederick Ndahani alisema watamkumbuka Rais Magufuli kwa kuwafundisha kuwa wazalendo wa Taifa letu.
" Vijana na baadhi ya watanzania tulikosa uzalendo lakini Magufuli akatuhasa na kutusihi tuwe wazalendo." alisema Ndahani.
Ndahani alisema kuonesha jinsi alivyo kuwa akiwapenda vijana alitoa nafasi nyingi za uongozi wakiwemo wakuu wa wilaya, mikoa na baadhi yao aliwateua kuwa mawaziri.
Alisema aliwateua vijana kwa sababu aliamini wanao uwezo wa kusimamia mambo kwa uchungu kwa kuwa wao ni nguvu ya Taifa.
Aidha Ndahhani alisema Rais Magufuli amefariki akiwa ametujengea uchumi wa viwanda na kutufikisha katika uchumi wa kati sambamba na elimu bure kwa wanafunzi wa shule ya msingi na Sekondari.
Alisema kwa niaba ya vijana wa mkoa huu wanatoa pole kwa Makamu wa Rais Samia Suluhu, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu, Wabunge, viongozi wote na watanzania wote kwa msiba huu mkubwa na kuwa wanamuomba mrithi wake Mungu amjalie aendeleze yale yote mazuri aliyoyacha.
Mwanaharakati wa masuala ya kijamii kwa ujumla mkoani hapa Stellah Mwagowa alisema Rais Magufuli aliwaaminisha vijana kuwa wanaweza kwani hapo awali hawakuweza kudhubutu kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika chaguzi mbalimbali.
"Magufuli alijenga misingi kwa vijana kugombea nafasi mbalimbali ambapo katika Bunge la 12 wapo wengi tofauti na miaka mingine"alisema Mwagowa.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Dung'unyi wilayani Ikungi mkoani hapa, Yahaya Njiku alisema Rais Magufuli ametuachia alama na vitu ambavyo tutakapo kuwa tunaviangalia hatutaweza kumsahau kutokana na kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere ambao utawasaidia vijana kupata ajira na wananchi kupata umeme wa uhakika.
Njiku alitaja miradi mingine aliyoianzisha kuwa ni reli ya kisasa, madaraja makubwa jijini Mwanza na Dar-es-saalamu, kununua vivuko kwa ajili ya usafiri wa majini pamoja na usafiri wa anga
Post A Comment: