SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limeungana na Taasisi ya Vijana Think Tank katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Watoto wa Kike katika Fani ya Sayansi kwa kuwawezesha wanafunzi wa kike kutoka shule ya sekondari Halisi kutembelea Mradi Mkubwa wa kuzalisha umeme kwa maji wa Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,115.


Lengo la safari hiyo ya kimasomo, ilikuwa ni kutoa hamasa zaidi kwa wanafunzi wa kike kuyapenda masomo ya sayansi na mwisho wa siku idadi ya wanafunzi wa Jinsia hiyo kupenda masomo ya sayansi kuongezeka. 


Akitoa ufafanuzi wa hatua mbalimbali za maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Mwl. Nyerere mbele ya wanafunzi hao, Mhandisi Dismas Mbote ambaye ni Msimamizi wa njia za maji pamoja na bwawa kwenye mradi huo amesema, masomo ya vitendo ikiwemo ziara za za kimasomo katika maeneo mbalimbali huwajengea uelewa zaidi katika masomo na hatimaye itapekea wanafunzi hususan wa kike kufurahia masomo ya sayansi.


Sambamba na hilo Mhandisi Mbote, ametoa rai kwa wanafunzi wa shule nyingine kwenda kutembelea Mradi huo kwa lengo la kujifunza na kusisitiza kuwa njia ya kujifunza kwa vitendo inakuza uelewa kwa walichokisoma darasani.


"Wanafunzi mara nyingi wanajifunza kwa kuona, Natoa rai kwa wanafunzi wa shule nyingine waje wajifunze bure, kujifunza kwa vitendo kunakuza uelewa kwa walichokisoma darasani" alisema Mhandisi Mbote


Kwa upande wake, Afisa Miradi Msaidizi wa Taasisi ya Vijana Think Tank (VTT), Bi. Fatma Mang'ena ametanabaisha kuwa, hadi sasa ni asilimia 30 pekee ya wanafunzi wa kike nchini ndio wamejikita katika masomo ya sayansi.


Na kuongeza kuwa, jitihada za makusudi zinapaswa kuchukuliwa kuitatua changamoto hiyo ikiwemo mikakati yao kama taasisi ya kuwepeleka wanafunzi katika miradi na maeneo mengi ili kujifunza kwa vitendo kama walivyofanya kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Halisi ya Jijini Dar es Salaam.

Aidha, Bi. Fatma amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuwawezesha na kufanikisha ziara hiyo ya kitaaluma kutembelea Mradi wa Mwl. Nyerere na kuongeza kuwa, wamejipanga kutekeleza jambo hilo walau mara moja kwa shule tofauti tofauti na maeneo na vitengo tofauti nchini ili kuleta hamasa kwa wanafunzi wa kike kuyapenda masomo ya sayansi.


Naye mmoja wa wanafunzi kutoka Shule ya sekondari Halisi, Rebecca Albert, amelishukuru Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Vijana Think Tank (VTT) kwa kuwawezesha kufika eneo la Mradi wa kuzalisha umeme wa Mwl. Julius Nyerere (JNHPP) ambapo amesema, wamepata fursa ya wao kujifunza kwa vitendo huku akitoa wito kwa wazazi kuwaruhusu watoto wao kushiriki safari za kimasomo zenye lengo la kujifunza hususan masomo yanayohusiana na sayansi ili kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike wanaosomea masomo na fani za sayansi nchini.


Katika ziara hiyo, wanafunzi wamejionea na kujifunza hatua mbalimbali za maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ikiwemo eneo la bwawa ambalo maji yatahifadhiwa kwa ajili ya kuzalisha umeme (main dam), handaki mchepuko (direction tunnel), eneo la kusagia mawe (crushing plants). Pamoja na mitambo mbalimbali ikiwemo ya kupeleka hewa (air compressor) eneo la mgodini.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: