Na Mwandishi wetu ,Mwanza
SERIKALI imesema kuwa itawapokonya na kutowapa tena kazi ya kujenga miradi ya maji Wakandarasi wazembe walioshindwa kuitekeleza kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi ametoa tamko hilo jana wakati wa ziara yake kwenye mradi wa maji wa vijiji vya Buyagu, Kalangalala na Bototo Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.
Tamko hilo amelitoa kufuatia taarifa ya utekelezaji na hali halisi aliyoishuhudia ya mradi huo ambapo alieleza kusikitishwa na Mkandarasi mzawa aliyekuwa akiutekeleza.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi, Meneja wa Wakala wa Maji vijijini (RUWASA) Sengerema, Mhandisi Cassian Wittike alisema ulikuwa ukitekelezwa na Mkandarasi mzawa Kampuni ya D4N Construction Limited ya Wilayani Kahama ambaye alishindwa kuukamilisha kwa mujibu wa mkataba wake.
"Mradi huu ni miongoni mwa miradi tuliyorithi kutoka kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa mwaka 2019 na haukua umekamilika kutokana na uwezo mdogo wa mkandarasi," alimueleza Naibu Waziri.
Mhandisi Wittike amesema kwamba mradi ulianza kutekelezwa tangu Desemba 2013 na ulipaswa kukamilika Juni, 2014 mwaka kwa gharama ya shilingi bilioni 1.7 lakini
"Mkandarasi aliyepewa jukumu alishindwa na hivyo tuliuchukua na kuanza kutekelezwa na wataalam wa RUWASA Sengerema kuanzia mwaka 2019 na sasa hivi tupo kwenye majaribio na umeanza kutoa majitulikuta haupo," alisema Mhandisi Wittike
Kufuatia maelezo hayo na hali halisi ya mradi aliyoishuhudia, Naibu Waziri Mahundi alisisitiza kwamba Serikali haitomvumilia mkandarasi mzembe na badala yake atapokonywa mradi na atawekwa kwenye orodha ya wakandarasi ambao hawana sifa ya kukabidhiwa kutekeleza miradi ya maji kote nchini.
"Mkandarasi atakayeshindwa kutekeleza mradi inavyopasa atanyang'anywa mara moja na hatopewa tena kazi nyingine, hapo ajue amejifuta na ameingia rasmi kwenye orodha ya wakandarasi wasiokuwa na sifa wala uwezo wa kujenga miradi ya maji," alisisitiza Mhandisi Mahundi.
Aliongeza kwamba hali ya uzembe wa baadhi ya wakandarasi hususan wazawa inamsikitisha Rais. Dkt. John Pombe Magufuli hasa ikizingatiwa kwamba dhamira yake ya kuwainua haileti tija kusudiwa.
"Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli anafarijika kuona wakandarasi wazawa wanapata kazi ya kujenga miradi lakini bahati mbaya baadhi yao kwa kukosa uzalendo wanamuangusha kwa kushindwa kutekeleza vyema miradi wanayokabidhiwa," alisema Naibu Waziri Mahundi.
Naibu Waziri Mahundi alisisitiza kwamba Serikali ameonya wakandarasi wote wenye tabia ya kutumia fedha wanazolipwa kwa ajili ya kutekeleza miradi na badala yake wanaipeleka kwenye masuala mengine yasiyohusiana na mradi.
"Wakandarasi mnapaswa kutambua fedha mnayolipwa ni kwaajili ya kujenga miradi na sio kufanyia matumizi mengine sasa bahati mbaya hua fedha hii mnaipeleka kwenye matumizi tofauti na hapa ni lazima mshindwe kutekeleza miradi kwa ubora uliyokusudiwa," alisisitiza Naibu Waziri Mahundi.
Mwisho.
Post A Comment: