VIJANA 283 kati ya 301 waliohitimu mafunzo ya Ukarimu na Utalii mwaka 2020 katika Chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii (VETA Njiro) jijini Arusha wamepata ajira.


Akipokea taarifa ya wahitimu hao katika Mahafali ya nane ya Chuo hicho iliyofanyika jijini Arusha tarehe 4 Desemba, 2020, Afisa Tawala wa Wilaya ya Arusha, Ndugu Nyangusi Nyailiba, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Arusha, alisema takwimu hizo zinathibitisha ubora wa mafunzo yanayotolewa na VETA na kuonyesha namna sekta ya Ukarimu na Utalii ina uhitaji mkubwa wa rasilimali watu yenye ujuzi na weledi.

“Takwimu hizi za wahitimu ambao wako kazini ni ushahidi wa ubora wa mafunzo yanayotolewa na chuo chetu na juhudi hizi zinaunga mkono dira ya nchi ya kujenga uchumi wa viwanda sambamba na kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Tano Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,”alisema.

Ndugu Nyailiba alihamasisha uongozi wa Chuo cha VETA Njiro kubuni mafunzo zaidi na kuongeza udahili kupitia mafunzo ya muda mfupi kwenye sekta ya hoteli na utalii ili kuweza kugusa na kubadilisha maisha ya wananchi wengi wa jiji la Arusha wanaotegemea sekta hiyo kujiingizia kipato.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema Mamlaka itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia ya chuo hicho ili kuwezesha chuo kuzalisha wahitimu wengi zaidi wa kuhudumia sekta ya utalii yenye mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi.

Alisema Mamlaka imeanza kazi ya upanuzi wa chuo hicho ambapo kwa mwaka 2020, kiasi cha shilingi milioni 647 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili, ukumbi wa mihadhara, maliwato pamoja na ukarabati wa majengo ya hoteli na utawala ya chuo hicho. Ujenzi huo umeanza na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2021.

Awali, Mkuu wa Chuo hicho, Ndugu Christopher Ayo, alisema wanafunzi 16 wamehitimu kwa ngazi ya stashahada, 218 Astashahada na 67 wamehitimu ngazi ya tatu ya Ufundi Stadi (NVA Level III).

Aliwasihi wahitimu hao kujikita zaidi kwenye eneo la kujiajiri ili waweza kuzalisha ajira kwa vijana wengine hasa kwa kuzingatia kuwa pamoja na mafunzo ya fani za hoteli na utalii, pia wahitimu hao walijifunza ujasiriamali, namna ya kutafuta masoko ya bidhaa pamoja na huduma kwa wateja .

Ayo alisema chuo hicho kimelenga kuongeza udahili kutoka wanachuo 411 kwa sasa hadi kufikia 700 ifikapo mwaka 2023.
Mmoja wa wahitimu wa chuo hicho, Amos Julius, alisema uwepo wa hoteli ya kisasa yenye hadhi ya nyota tatu (Three Stars Hotel) chuoni hapo mahsusi kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi imesaidia sana wanafunzi kuweza kufanya mazoezi kwa vitendo mara nyingi zaidi na kuwaongezea ujasiri katika kufanya kazi kwenye sekta ya hoteli na utalii.

Chuo cha VETA Njiro kilianzishwa mwaka 2011 na kinatoa mafunzo ya muda mrefu katika fani za Upishi,Huduma ya Mauzo ya Vinywaji na Chakula, Usafi wa Nyumba na Udobi, Uongozaji Watalii ,Usimamizi wa Uendeshaji wa shughuli za Utalii, Mapokezi Huduma za Malazi na Sanaa ya Mapishi.

Chuo pia kinatoa mafunzo ya muda mfupi katika fani mbalimbali ikiwemo Upambaji, Usafi wa majengo na maeneo ya wazi, Upishi, Huduma ya uuzaji vinywaji, uandaaji wa keki na mafunzo ya uongozaji watalii.
Share To:

Post A Comment: