Na. Majid Abdulkarim, Dodoma


Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw.Victor Kategere ametoa wito kwa Chama cha Akiba na Mikopo cha Mitaa kuhakikisha kinatoa mikopo kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya wanachama.


Wito huo ameutoa leo Jijini Dodoma katika ufunguzi wa Kikao cha chama hicho na kutaka wanachama kufanya urejeshaji kwa wakati na kuwa na ushiriki mzuri katika uchangiaji wa chama hicho ili chama kiweze kusimama imara na kuwa msaada kwa wanachama wake.


“Na imani kila mwanachama anaelewa faida ya kujiunga katika chama chenu hivyo basi mwendelee kuchangia na kushirikiana kwa karibu kwa kuweka na kukopa ili chama kidumu”, amesisitiza Bw.Kategere.


Vile vile Kategere amesema kuwa wanachama hao wanatakiwa kufanya huamasishaji mzuri kwa watu wengine ili kuongeza idadi ya wanachama na kufanya chama kuwa na idadi nzuri ya wanachama na kupata maendeleo Zaidi.


Aidha Mwenyekiti wa chama hicho Bw. Swedi Zidiheri amesema kuwa kwa sasa bodi hiyo ipo kwenye mchakato wa kufanya usajili kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Benki kuu ya Tanzania.

“Na hii ni kwa mujibu wa sheria mpya ya fedha inayotaka taasisi zote zinazohusika na masuala ya fedha zisajiliwe”, ameeleza Bw. Zidiheri.


Bw. Zidiheri ameongeza kuwa wamefanikiwa katika kutoa mikopo kwa wanachama walioomba na kukidhi vigezo vilivyowekwa na hesabu za chama zimekaguliwa kuishia mwaka 2019.


Pia Bw. Zidiheri ametoa shukrani kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Nyamhanga ambaye ni mwajiri kwa kuwapatia Ofisi kwa ajili ya shughuli za chama jambo ambalo limewapunguzia gharama za kulipia pango nje ya ofisi.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: