Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar Kunenge amemuelekeza Mkandarasi wa Kampuni ya Nyanza inayojenga barabara na Daraja la Kivule kuhakikisha ifikapo September 30 daraja hilo linakamilika na kuanza kutumika ili kupunguza kero ya usafiri kwa wananchi.

RC Kunenge ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya Ujenzi wa miundombinu Wilaya ya Ilala na Temeke ambapo ameonyesha kuridhishwa na hatua ya ujenzi ilipofikia na kuwataka waongeze juhudi.

Aidha RC Kunenge amesema ujenzi wa Madaraja hayo unaenda sambamba na ujenzi wa Barabara ya Kuelekea Hospital ya Wilaya ya Ilala iliyopo Kivule ambapo amewasisitiza TANROAD na TARURA kusimamia vizuri miradi hiyo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Akiwa kwenye ukaguzi wa Barabara ya Mbosi RC Kunenge amemuelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke kuhakikisha anatoa fedha za kumalizia ujenzi wa Barabara hiyo ili ikamilike ndani ya mwezi mmoja.
Pamoja na hayo RC Kunenge amesema tayari amewaelekeza Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo kuhakikisha wanatoka maofisini na kwenda kusikiliza kero za wananchi pamoja ukaguzi wa miradi ya maendeleo.


Share To:

Post A Comment: