Na John Walter-Babati
Taasisi ya
kuzuia na kupambana na Rushwa, imewaonya viongozi wa chama cha Mapinduzi (CCM) ambao wanaondoa majina ya wapiga kura halali
wa kura za maoni na kubandika majina ambayo wanaamini watawapigia kura wagombea
ambao wanawataka.
Wito huo
umetolewa leo Julai 16,2020 na Mkuu wa Takukuru Manyara Holle Makungu baada ya
kupata taarifa kwamba baadhi ya viongozi wa chama hicho tawala ngazi ya kata
wamekuwa na mtindo huo jambo ambalo ni kinyume na taratibu.
Hata
hivyo kufuatia hatua hiyo, Makungu amewasambaza
Makachero wa Takukuru kufanya uhakiki wa
majina halali kwenye maeneo yanayolalamikiwa.
Makungu
amewaambia viongozi wa Chama cha Mapinduzi wanaofanya mabadiliko hayo, wafahamu
kuwa hawako juu ya sheria na kwamba kitendo hicho cha kubadilisha majina ya
wapiga kura ni kosa la kughushi ambalo likithibitishwa adhabu yake kwa mujibu
wa Kifungu cha 337 Penal Code ni miaka saba jela.
Aidha amesema
kuwa makosa ya rushwa katika kipindi cha Uchaguzi yameanishwa katika vifungu
vya 21, 22 na 23 vya sheria ya Gharama za uchaguzi namba 6/2010 ambavyo ni
pamoja na hongo ya fedha kwa wapiga kura ili kuwashawishi kupiga au kutopiga
kura , ahadi za ajira kwa wapiga kura kwamba nitakuajiri kwenye ofisi Fulani,
kutoa zawadi, mikopo isiyo na riba au riba iliyo kinyume cha sheria.
Pamoja na
hayo amesema makosa hayo pia yanamhusu mpiga kura anayekubali kupokea fedha,zawadi,
mikopo, ahadi ya ajira au kitu chochote cha thamani ili ampigie kura au asipige
kura kwa mgombea.
Ameongeza
kuwa ni kosa pia kutoa vyakula, vinywaji kwa nia ya kushawishi wapiga kura,
sheria ambayo inaanza kufanya kazi kuanzia wakati wa mchakato wa wagombea ndani
ya vyama vyote vya siasa hadi wakati wa uchaguzi mkuu hapo Oktoba 2020.
Ametoa onyo
kwa Viongozi hao wa kata warejeshe majina ya wapiga kura za maoni ambao ni
halali mara moja na kuwataka makatibu wa wilaya wa chama cha Mapinduzi kutoa
ushirikiano kwa makachero wao wanaoshugulikia uchunguzi huo kubaini wachache
wanaotaka kurejesha demokrasia nyuma.
Post A Comment: