Nyumba Nzuri

Nyumba ni hitaji muhimu kwa watu wote. Kila mmoja anatamani na ana ndoto za kununua au kujenga nyumba nzuri na ya kisasa. Ni kweli kuwa ujenzi wa nyumba unahitaji rasilimali nyingi hasa fedha.

Pamoja na gharama hizi za ujenzi wa nyumba bado watu wengi wamekuwa wakishindwa kupata nyumba nzuri huku wakiwa tayari wamepoteza kiasi kikubwa cha pesa. Ni wazi kuwa yapo makosa mbalimbali yanayosababisha hali hii yakiwemo yale ya ukosefu wa elimu pamoja na uzembe wa aina mbalimbali.

Karibu ufuatilie makala hii ili uweze kufahamu makosa 8 unayoweza kuyaepuka wakati wa kujenga nyumba ili hatimaye uwe na nyumba bora.

1. Kutozingatia kanuni za kununua kiwanja

Watu wengi hawafahamu mambo muhimu ya kuzingatia wakati wanaponunua kiwanja. Hivyo hujikuta wakiingia katika matatizo mbalimbali kama vile kuvunjiwa nyumba zao, kujenga kwenye maeneo mabaya kama matindiga na mikondo ya maji. Ni muhimu kuhakikisha mambo yafuatayo kabla na wakati wa kutafuta kiwanja cha kujenga nyumba:
  • Kiwanja hakina umiliki zaidi ya mtu mmoja
  • Kiwanja hakina mgogoro wa kisheria
  • Kiwanja hakiko kwenye hifadhi ya barabara au mazingira
  • Kiwanja kinafaa kwa ujenzi (Siyo tindiga, eneo la magadi, eneo la maporomoko ya ardhi au mkondo wa maji)

Ukizingatia haya utaweza kupata kiwanja kizuri kwa ajili ya kujenga nyumba bora kwa ajili ya matumizi yako.

2. Uchaguzi duni wa ramani

Mara nyingi mtu humwita fundi na kumwambia kuwa “nataka unijengee nyumba ya vyumba vitatu”. Fundi anapouliza ramani yako iko wapi wao husema we angalia tu nzuri alimradi iwe ya vyumba vitatu. Hili ni kosa kubwa sana kwani husababisha watu wengi kujengewa nyumba ambazo hawazipendi.
Ramani nzuri kwa fundi inaweza isiwe nzuri kwako na familia yako. Zingatia uchaguzi wa ramani kwa makini kulingana na wewe unavyopenda, hili litakufanya pia upende nyumba itakayojengwa.Ramani
Ramani mbaya.

3. Kutokufanya makadirio sahihi

Ni wazi kuwa umeona nyumba nyingi zikianzwa lakini hazimaliziki. Hili kwa kiasi kikubwa linatokana na kufanya makadirio na maandalizi duni kabla ya kuanza kujenga. Ujenzi wa nyumba unahitaji maandalizi mazuri hasa kifedha. Ni muhimu kujiandaa vyema kabla ya kuanza ujenzi ili usikwamie njiani.
Mambo unayoweza kufanya:
  • Weka makadirio ya gharama za ujenzi ili angalau uandae kiasi fulani cha pesa.
  • Nunua baadhi ya vifaa kabla. Unaweza kununua mchanga, mawe, kokoto, nondo, mabati n.k. Ili kupunguza matumizi ya pesa wakati wa ujenzi.
  • Weka mipango ya kutunza mahitaji yako mengine ya pesa kabla ya kuanza ujenzi. Kwa mfano ada za shule, kodi mbalimbali, chakula n.k.
  • Punguza matumizi yasiyokuwa ya lazima kabla na wakati wa ujenzi. Ikumbukwe kuwa pesa nyingi zitahitajika kwenye ujenzi.

4. Kutokubainisha mahitaji

Mahitaji ya nyumba hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Hivyo ni vyema ukabainisha mahitaji yako kwa nyumba husika. Nimeshuhudia watu wakijenga nyumba na kuzivunja ua kuzifanyia marekebisho kila mwaka kutokana na kutobainisha mahitaji yao mapema.
Kurekebisha au kuvunja na kujenga upya nyumba yako kutakupotezea kiasi kikubwa sana cha pesa. Kwa mfano wengi hurekebisha nyumba zao ili kuongeza vitu kama vile jiko, choo na bafu, milango, madirisha n.k. ambavyo wangepanga mapema wangekuwa wameviweka mwanzoni.

5. Kutokuwaza mbeleni

Ni vyema kuwaza mbeleni kwani nyumba ni kitu utakachokitumia muda mrefu. Ni vyema ukafahamu vitu na mahitaji utakayoyataka kwenye nyumba yako kwa siku za mbeleni. Hili litakuwezesha kujenga nyumba utakayoitumia na kuifurahia kwa muda mrefu zaidi.
Ni vyema pia ukawaza kuweka miundombinu ya kisasa kama vile umeme, simu (intercom), nyaya za televisheni, Kiyoyozi, na hata Data. Hata kama huna pesa za kuweka mambo haya unaweza kubuni nyumba ambayo baadaye itaruhusu miundombinu hii.Nyumba
 
Nyumba ya Kisasa

6. Kutumia mafundi duni

Wengi hupenda kuokoa gharama kwa kutumia mafundi wenye uwezo mdogo ili wawalipe kwa bei nafuu. Ni wazi kuwa rahisi inaumiza. Jiande vyema kabla ya ujenzi ili uweze kuitendea haki nyumba yako kwa kutumia mafundi bora wanaoimudu kazi yao vyema. Kutumia mafundi bora kutakufanya kupata pia kazi yenye ubora.Nhazi
Ngazi zilizokosewa.

7. Kupuuza kanuni muhimu za ujenzi

Ujenzi una kanuni zake mbalimbali ambazo ni vyema zikazingatiwa. Kutokana na uelewa mdogo, watu wengi hawazingatii kanuni muhimu za ujenzi kama vile kumwagilia maji yakutosha pamoja na kujenga nyumba kulingana na muda.
Nimeshuhudia nyumba nyingi zikivunjika kutokana na kujengwa haraka haraka bila kutoa muda wa kutosha kwa nyumba kukomaa na kustahimili uzito. Pia nimeona watu wakipuuzia umuhimu wa kunyesha sehemu iliyojegwa kwa maji mengi; ni muhimu kunyesha vyema eneo lililojengwa kwani “uimara wa saruji ni maji”; unaweza kunyesha angalau kwa siku saba asubuhi na jioni.Nyumba iliyoporomoka
 
Nyumba iliyoporomoka kutokana na kupuuza kanuni za ujenzi.

8. Matumizi ya vifaa duni

Kama nilivyoeleza katika maelezo yaliyotangulia, uhaba wa fedha huwafanya watu wengi kufanya kazi duni. Hivi leo kuna vifaa mbalimbali vya ujenzi, lakini si vyote ni bora. Kwa mfano, hakuna haja ya kununua kitasa kinachovunjika baada ya mwezi au vigae vinavyofubaa. Kwa kufanya hivi utapoteza pesa nyingi kwa kununua vifaa hivyo mara kwa mara. Jibane, jipange ufanye kitu cha uhakika.

Hitimisho

Ni wazi kuwa ujenzi wa nyumba ni shunguli pevu inayohitaji kutulia, moyo na maandalizi stahiki. Hakuna kitu kinachoshinda nia na mipango mizuri. Naamini kwa kuyaepuka makosa tajwa hapo juu utaweza kujenga nyumba bora, salama na ya kisasa kabisa.
Je umeshajenga nyumba yako? Ulipata changamoto gani na ulizitatuaje? Tafadhali tushirikishe kwa kutoa maoni yako hapo chini. Pia usisahau kulike ukurasa wetu wa Facebook pamoja na kuwashirikisha wengine makala hii.
Share To:

Post A Comment: