Ramadhan Hassan -Chemba
MKUU wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Asia Abdallah, amesema hatua kali zitachukuliwa kwa wazazi watakaokiuka agizo la kutowapeleka watoto wao shule katika wilaya za Chemba na Kondoa.
Akizungumza juzi katika Kijiji cha Magadi, Kata ya Soya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma wakati wa sherehe za Maulid, Asia alisema hakuna kisingizio  cha kutokumpeleka mtoto shule kwani Serikali imeondoa vikwazo vyote ikiwemo ada na michango mingine mashuleni.
 “Rais anapeleka mabilioni ya fedha kila mwezi, zaidi ya Sh bilioni 23 kwa ajili ya watoto wetu wapate elimu bila malipo, zamani  sisi tulikuwa tunasoma tunajilipia ada, sasa hivi hakuna,” alisema Asia.
Vilevile aliwataka viongozi wa dini wa wilaya hizo  kuwahamasisha waumini na wananchi kujitokeza kwa wingi  kumpigia kura Rais John Magufuli katika Uchaguzi Mkuu  wa Oktoba ili kuleta maendeleo chanya kwa taifa.
Alisema katika historia, wilaya za  Chemba na Kondoa  kuna changamoto ya watu kutokujitokeza kupiga kura  hivyo ni jukumu lao sasa kupambana kumpigia kura Rais Magufuli.
“Kila mwananchi akitambua wajibu wake tutafika mbali sana, Rais wetu anafanya kazi ngumu sana  na kama mnafuatilia habari mbalimbali kwenye Tv, redio na  mitandao ya kijamii utaona nchi hii ilikuwa masikini  na ilipanga kufikia uchumi wa kati 2025  na kabla haujafika tayari  tumeingia kwenye  uchumi wa kati, ni dhahiri  nchi hii siyo masikini, tunahitaji viongozi wa aina ya kina Magufuli, na wananchi tushirikiane kwa pamoja ili tuondokane na wimbi hii la umasikini,” alisema Asia.
Alitoa rai kwa  mashekhe  na jamii kwa ujumla  kufanya kazi kwa bidii na kuachana na mambo yasiyokuwa na tija  ili kuleta heshima kwa taifa.
Asia alisema alikuwa na mpango wa kutia nia kugombea ubunge  wa Viti maalumu  Mkoa wa Dodoma, lakini ameshindwa kutokana na kutii mamlaka ya rais kwakuwa bado anahitaji kuendelea kumsaidia katika majukumu yake ya kufanya kazi katika Wilaya ya Kilolo.
“Katika vitabu vya dini mnatambua tumeelekezwa kutii mamlaka, hivyo nimetii mamlaka ya uteuzi wangu, mimi ni nani mpaka niwe na kiburi mbele ya kiongozi wangu nisitii mamlaka,’’ alisema Asia.
Naye, mwalimu wa madrasa, Aisha Mohamed aliwataka  wazazi kuwalea watoto wao katika maadili mema ili kuwa na kizazi chenye utii siku za mbeleni.
Share To:

Post A Comment: