Mkuu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Nico Livingstone akiongea na wahudumu,wamiliki wa bara na wamiliki wa nyumba za kulala wageni(hawapo picha)jana alipokutana nao kwa ajili ya kujadiliana namna ya kuweka usalama sehemu za starehe ili kukabiliana na matukio ya uharifu na waharifu ambao wameanza kufanya vitendo hivyo katika baadhi ya maeneo ambapo wahudumu wa Bara ni wahanga wakubwa wa vitendo hivyo,katikati mkuu wa kituo cha Polisi Tunduru Jamal Ibrahim na kulia Mkuu wa kikosi cha Usalama barabara John Ntude.


JESHI la polisi wilayani Tunduru limekutana na wahudumu,wamiliki wa Bara pamoja na wamiliki wa nyumba za kulala wageni ili kwa pamoja kupanga mkakati wa kudhibiti vitendo vya uharifu na waharifu sehemu zao za kazi. 


Akizungumza na wahudumu hao jana, Mkuu wa Jeshi la Polisi wilayani humo Nico Livingstone alisema, suala la ulinzi la mwananchi na mali ni la kila mmoja na sio taasisi moja. Amewataka wahudumu na wamiliki wa bara na nyumba za kulala wageni kutoa taarifa kwa polisi pale wanapohisi kuwepo kwa dalili za uharifu katika maeneo yao ya kazi. 


Alisema, hatua hiyo itawasaidia wahudumu hao kiusalama kwani wanakutana na watu wengi katika shughuli zao za kila wakiwemo waharifu na wale ambao sio waharifu kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini hata nje ya nchi. 


Kwa mujibu wa mkuu wa polisi wilaya, suala la ulinzi ni lazima lianzie kwa mtu mmoja mmoja,kwa hiyo vizuri kuwepo ushirikiano kati ya jeshi la polisi na jamii mzima badala ya jukumu hilo kuachwa kwa polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama. 


Aidha,amewataka kutokubali kutumika na wanasiasa uchwara wasio itakia mema wilaya hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu, kwani kuna uwezekano baadhi yao wanataka kutumia mgongo wa uchaguzi kama sehemu ya kutimiza malengo yao. 


“tunakwenda katika uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu, lakini Tunduru isipokuwa salama hatuwezi kusema tunahitaji Uchaguzi huru na wa haki,nawambeni san sana kamwe msikubali kutumika na wanasiasa uchwara ambao watachafua sifa mzuri ya wilaya yetu ya Tunduru”alisema OCD Nico. 


Baadhi ya wahuduma wa Bar wameliomba jeshi la polisi kuongeza ulinzi kwenye maeneo hayo hasa nyakati za usiku ambapo waharifu wanatumia muda huo kuwajeruhi, kupora fedha na simu wahudumu na wateja wanaokwenda kupata huduma. 


Siwema Zuberi muhudumu wa Bar ya Terminal amelalamikia baadhi ya wateja kuwafanyia wahudumu vitendo visivyokuwa vya uungwana kama kuwapora, kuwajeruhi na wakati mwingine kuwaingilia kinyume cha maumbile pindi wanapokuwa chumbani licha ya kuwepo makubaliano kati yao. 


Ameliomba Jeshi la polisi kuweka doria mara kwa mara kwenye bar na nyumba za kulala wageni kwani maeneo hayo ndiko ambako matukio mengi ya uharifu yanakofanyika nyakati za usiku. Aidha Siwema, ameishukuru serikali kwa kuwatambua wahudumu na kazi yao tofauti na baadhi ya watu wachache wenye fikra ovu kwamba wahudumu ni watu wasiokuwa na mchango wowote katika jamii licha ya ukweli kwamba kazi wanazofanya zinachangia mapato ya Serikali. 


Julieth Chabuluma mfanyabiashara wa chakula katika Bar ya Amazon ameomba kuwe na utaratibu wa waendesha boda boda kila kijiwe kuvaa sale maalum zenye namba ili wanapofanya vitendo vya uharifu waweze kutambulika mara moja. 


Alisema, baadhi ya waharifu wanatumia kazi ya bodaboda kama sehemu ya kujificha ambapo ameshauri ni vema kila mwendesha boda boda atambulike kwa kuvaa sale.
Kwa upande wake,mkuu wa kikosi cha usalama barabarani(DTO)wilayani humo aliyefahamika John Ntude alisema, tayari polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani limeweka utaratibu maalum kwa waendesha boda boda kuwa na sale kama sehemu ya usalama wa wateja na wao wenyewe.
Amewatahadharisha wahudumu wa bar kuchukua tahadhari pindi wanaporudi nyumbani kwa kuwa na dereva mmoja mwaminifu badala ya kupanda kila bodaboda.
Share To:

Post A Comment: