Na. Ramadhani Kissimba na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imeamua kuziunganisha Benki ya TPB na TIB Corprate kuanzia Juni Mosi, 2020 kwa lengo la kuboresha utendaji wa benki inazomiliki ili kuwa na Benki moja ya biashara ambayo ni imara.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka, katika Mkutano na Waandishi wa Habari.
Bw. Mbuttuka alisema kuwa muungano wa Benki hizo unalenga kuleta mageuzi makubwa ya kiutendaji, kimfumo, kimuundo na taswira ili benki hiyo iweze kuhimili ushindani wa kibiashara kwenye sekta ya fedha.
“Serikali inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kuhakikisha utendaji wa benki zake unaimarika na maslahi ya wenye amana na wateja wote yanalindwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa Benki na taasisi za fedha”, alieleza Bw. Mbuttuka
Bw. Mbuttuka alisema kuwa  kwa hatua ya awali, Benki ya TPB itachukua mali na madeni ya Benki ya TIB Corprate na Wateja wote wa Benki ya TPB na Benki ya TIB Corporate wataendelea kuhudumiwa kwenye matawi yao ya sasa hadi hapo watakapotaarifiwa vinginevyo.
Aidha alisema kuwa Serikali inawahakikishia wateja wa benki hizo mbili pamoja na umma kuwa huduma za kibenki hazitaathirika kwa vyovyote vile kutokana na mabadiliko hayo
Serikali  imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha utendaji wa mashirika na taasisi za umma ikiwemo kuunganisha taasisi zinazotekeleza majukumu yanayofanana, ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
Share To:

Post A Comment: