Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella akifungua kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Tanga kilichofanyika Septemba 23, 2019 kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Korogwe kulia ni katibu tawala wa mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Saidi kushoto ni Mkuu wa wilaya ya korogwe Kissa Gwakisa (Picha na Yusuph Mussa)
 Wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Tanga kwenye kikao kilichofanyika Septemba 23, 2019 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Korogwe. (Picha na Yusuph Mussa)
 Wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Tanga kwenye kikao kilichofanyika Septemba 23, 2019 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Korogwe. (Picha na Yusuph Mussa)
Wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Tanga kwenye kikao kilichofanyika Septemba 23, 2019 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Korogwe. (Picha na Yusuph Mussa)

Na Yusuph Mussa, Korogwe


KAMATI ya Afya ya Msingi Mkoa wa Tanga imetakiwa kusaidia kukanusha upotoshaji unaoweza kujitokeza kutokana na kampeni ya chanjo mbalimbali zinazofanyika nchini, lakini pia kutoa taarifa sahihi kwa wananchi pale panapotokea upotoshaji kuhusu chanjo hizo.


Lakini pia  kuelimisha jamii kuhusu kampeni shirikishi ya chanjo ya Surua na Rubella, kuhamasisha ushiriki wa jamii ikiwemo viongozi, wazazi na walezi kuhakikisha kila mlengwa anafikiwa katika eneo husika.


Hayo yalisemwa jana Septemba 23 na Mratibu.wa Chanjo Mkoa wa Tanga Seif Shaibu kwenye kikao cha Afya ya Msingi Mkoa wa Tanga, ambapo Mwenyekiti wake ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe. 


Shaibu alitolea mfano kuwa baadhi ya chanjo zinazotolewa kama vile ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi wanayopewa wasichana wenye umri wa miaka 14, ambapo baadhi ya wananchi wanadai chanjo  hiyo inaua kizazi. Pia watoto wanaougua surua wanafungwa kamba na kuelezwa huyo ni pepo mchafu atapita.


"Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Tanga inatakiwa kuelimisha jamii kuhusu kampeni shirikishi ya chanjo ya Surua na Rubella, kuhamasisha ushiriki wa jamii ikiwemo viongozi, wazazi na walezi kuhakikisha kila mlengwa anafikiwa katika eneo husika.


"Pia kusaidia kukanusha upotoshaji unaoweza kujitokeza kutokana na kampeni ya chanjo au chanjo kwa ujumla wake, na kutoa taarifa sahihi kwa wananchi pale panapotokea upotoshaji kuhusu chanjo. Kuhamasisha viongozi wengine kushiriki katika uhamasishaji kwenye maeneo yao ya utendaji kazi kila siku ili walengwa wote waweze kufikiwa" alisema Shaibu.


Akitoa elimu mbele ya wajumbe wa kikao hicho ambao ni wakuu wa wilaya, wakurugenzi, makatibu tawala wa wilaya, viongozi wa dini, waganga wakuu wa wilaya, wataalamu na wadau wengine, Shaibu alisema surua ni ugonjwa unaosababishwa na virusi aina ya Morbillivirus paramyxvirus vinavyoenea kwa haraka.


Alisema ugonjwa huathiri watu wa rika zote, lakini watoto wenye umri chini ya miaka mitano huathirika zaidi. Ugonjwa wa surua huenezwa kwa njia ya hewa hasa pale mgonjwa anapokohoa ama kupiga chafya, na maambukizo huwa ni ya haraka sana, hasa sehemu zenye msongamano.


"Dalili za ugonjwa wa surua siku chache za mwanzo mtoto huwa na homa, mafua na kikohozi, macho yanakuwa mekundu na hutoa majimaji, vipele vidogo hutokea ambavyo huanza kwenye paji la uso, nyuma ya masikio na kusambaa usoni na mwili mzima. Na madhara ya ugonjwa wa surua ni masikio kutoa usaha ambao huweza kusababisha kutokusikia. Vidonda vya macho vinaweza kusababisha upofu, nimonia, utapiamlo, kuvimba ubongo na kifo" alisema Shaibu.


Shaibu pia alizungumzia ugonjwa wa rubella  na dalili zake ambao unasababishwa na virusi vya rubella na huenezwa kwa njia ya hewa. Mara nyingi huwapata watoto wadogo ingawa unaweza kumpata mtu wa rika yeyote kwa mfano mama mjamzito, ambapo mama mjamzito mwenye maambukizi ya virusi vya rubella huweza kumuambukiza mtoto aliye tumboni, na dalili zake hufanana na surua mfano vipele vidogo vidogo, homa, macho kuwa mekundu, uchovu wa mwili, vidonda kooni, uvimbe kwenye matezi na mafua.


"Athari za ugonjwa wa rubella ni kuwa ugonjwa huu ukimpata mama mjamzito unaweza kuleta madhara yafuatayo kwa mtoto. Nayo ni mtoto wa jicho, matatizo ya moyo, kutokusikia vizuri, mtindio wa ubongo na matatizo ya ukuaji wa mwili. Kwa mtu mzima anaweza kupata madhara kama maumivu ya viungo, upungufu wa chembe hai nyeupe, maambukizi kwenye ubongo na mishipa ya fahamu na kuzaa njiti au kifo" alisema Shaibu.


Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Jonathan Budenu alisema lengo kuu la kampeni ya kitaifa ni kuzuia na kupambana na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ambayo ni ugonjwa wa surua, rubella na polio kwa kutoa chanjo kwa watoto wote wenye umri wa miaka mitano.


Dkt. Budenu alisema kampeni hiyo ina lengo la kuongeza kinga kwa watoto wote kwa kuwapatia chanjo hata kama wameshapata chanjo hizo katika utaratibu wa kawaida wa kutoa huduma za chanjo.


Shegela alisema viongozi wa Serikali, dini na wale wa mitaa na vijiji wanatakiwa kushiriki kwenye kampeni hiyo ya chanjo ya surua- rubella kwa kwenda kusaidia kutoa elimu ya chanjo zinazotolewa na Serikali. 


MWISHO.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: