Mkuu mpya wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare  amewataka viongozi na watendaji wa ngazi mbalimbali katika Mkoa wa Morogoro kumsaidia Rais John Magufuli kukabiliana na kuzitatua kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wanyonge.

Pia amewataka na kujitafakari upya kila mmoja kwa nafasi yake kilichosababisha Rais akatengua uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Kebwe Stephen Kebwe.

Sanare alisema hayo baada ya kukabidhiwa rasmi nyenzo zikiwamo taarifa na nyaraka mbalimbali za mkoa kutoka kwa Kebwe Stephen, ambapo akawataka watendaji na viongozi hao kushirikiana na kuhakikisha anatambua kuwa yupo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na sio vinginevyo.

Sanare alisema atakuwa tayari kuwahudumia wananchi ndani ya saa zote 24 kila siku katika nafasi hiyo.

Alisema changamoto kubwa inayoonekana mbele yake na iliyotajwa hata na Rais ni migogoro ya ardhi inayohusisha wakulima na wafugaji, ambapo alisema licha ya yeye kutoka jamii ya wafugaji, hatakuwa mkuu wa mkoa wa jamii ya wafugaji, bali ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambao ni wa jamii ya Watanzania wote.

 “Sitakuwa na simile kwa yeyote atakayevunja sheria na taratibu zilizopo, kama ni Masai kakosea, huwa tunajua pia namna zetu za kuwajibishana na kwenye hili la migogoro ya wakulima na wafugaji itabidi kwanza nijue tatizo ni nini, mbona zamani makundi yote yaliishi pamoja, kulikoni sasa hivi na kila mwenye haki atapata haki yake bila kujali kabila lake,” alisema
Share To:

msumbanews

Post A Comment: