Na Ismail Ngayonga-MAELEZO
SEKTA
ya Kilimo imeendelea kuwa ni Sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa
wananchi na Taifa kwa ujumla hususan katika kipindi hiki tunapojizatiti
kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.
Kilimo
kimeendelea kuimarika na hivyo kuchangia asilimia 30.1 katika Pato la
Taifa kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 29.2 kwa mwaka 2016
pamoja na kuchangia ajira wananchi kwa asilimia 65.5 na kuchangia
malighafi za viwanda kwa asilimia 65.
Serikali
kupitia Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta
zinaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wakulima na wafanyabiashara na
kuboresha miundombinu wezeshi ili kuwezesha upatikanaji wa chakula na
masoko ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi katika maeneo yote.
Huduma
za Ugani ni muhimu sana katika kufikisha na kuelekeza wakulima,
wafugaji na wavuvi mbinu bora za kuongeza tija katika uzalishaji, ubora
wa mazao kwa usalama wa chakula na lishe pamoja na upatikanaji wa
malighafi za viwanda vinavyotegemea kilimo, mifugo na uvuvi.
Aidha,
huduma za Ugani hapa nchini zinatolewa kupitia mifumo mbalimbali
ikiwemo ubinafsishaji, mikataba, sekta ya umma na binafsi, ugatuaji wa
huduma za ugani na utandawazi wa soko huria. Baada ya ugatuaji wa
madaraka (1997) majukumu ya kutekeleza huduma za ugani yalihamishiwa
Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
Baada
ya ugatuaji wa huduma za ugani kumekuwako na changamoto mbalimbali za
kiutendaji ikiwemo Ufuatiliaji na uratibu wa huduma za ugani katika
Halmashauri umekuwa na mapungufu kwani hakuna uwajibikaji wa moja kwa
moja wa wataalam wa Kilimo walioko Halmashauri na Wizara ya Kilimo
pamoja na Halmashauri kutoajiri wataalamu wa kutosha wa ugani, kutotoa
motisha kwa kuwaendeleza watumishi wake hivyo kuathiri utoaji wa huduma
za ugani.
Ili
kufikia malengo iliyoyaweka katika Sekta ya Kilimo nchini, Serikali
kupitia Wizara ya Kilimo ilizindua Programu ya Kuendeleza Sekta ya
Kilimo Awamu ya Pili (2017/2028), ambayo inalenga kuleta mageuzi katika
Sekta ya Kilimo ambapo utekelezaji wake utazingatia kuimarisha utafiti,
huduma za ugani na mafunzo; upatikanaji wa masoko ya mazao na
miundombinu ya uzalishaji.
Akiwasilisha
Hotuba ya Makadiro ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020,
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga anasema Serikali imeendelea kuboresha
vyuo na vituo vya mafunzo ya kilimo ili kukidhi mahitaji ya wataalam wa
ugani kilimo katika ngazi ya kijiji na kata.
Anasema
kuwa Katika mwaka 2018/ 2019, Wizara kupitia vyuo vyake 14 vya kilimo
imedahili na kufundisha wanafunzi 2,389 ambapo wanafunzi 2,051
wamefadhiliwa na Serikali ambapo wanafunzi 1,537 ni ngazi ya Astashahada
na 852 ni ngazi ya Stashahada na jumla ya wanafunzi wanafunzi 1,026
wakiwemo 263 wa Stashahada na 763 wa Astashahada wamehitimu masomo yao
mwezi Juni, 2019.
“Vyuo
hivyo vinatoa Astashahada na Stashahada za Kilimo Mseto, Stashahada ya
Umwagiliaji, Matumizi Bora ya Ardhi, Uzalishaji Chakula na Lishe,
Matumizi ya Zana za Kilimo, Uzalishaji wa Mazao, Mboga, Maua na Matunda”
anasema Waziri Hasunga.
Waziri
Hasunga anasema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la
Lutheran World Relief (LWR) kupitia mradi wa Invest imehuisha mtaala wa
Kilimo Mseto na kuzalisha mtaala mpya wa kilimo (Agriculture Production)
ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kutimiza masharti ya Baraza la
Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Akifafanua
zaidi Hasunga anasema mradi wa Invest umejenga kitalu nyumba katika
Chuo cha Taifa cha Sukari Kidatu ili kutoa mafunzo bora kwa wagani
tarajali na wakulima na kuwajengea uwezo wakufunzi 20 kutoka vyuo vya
Kilimo Ilonga (Kilosa), KATRIN (Ifakara) na Chuo cha Taifa cha Sukari
Kidatu ili wafundishe kwa kufuata mwongozo wa mfumo wa moduli.
Anaongeza
kuwa Serikali kupitia Wizara ysa Kilimo imeendelea kuwajengea uwezo
wakufunzi wa kilimo 22 ambapo wakufunzi 10 wapo katika mafunzo ya
Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) na 12
wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi nchini India na China pamoja na
kushirikiana na Taasisi Binafsi kuandaa na kuendesha mafunzo ya muda
mfupi ya kuwajengea uwezo wakulima kuhusu teknolojia mbalimbali za
kilimo.
Kwa
mujibu wa Hasunga anasema Mafunzo hayo yalihusu Kilimo cha Korosho,
Mtwara (wakulima 67), Kilimo cha Mahindi na Maharage, Ukiriguru
(wakulima 51), Usindikaji wa mazao- Uyole (wakulima vijana 56), na
Kilimo bora cha soya (wakulima 31), Kilimo shadidi cha mpunga (wagani
33), kilimo bora cha alizeti (wakulima 25 na wagani 5), na kilimo bora
cha mpunga (wakulima 20), Ilonga.
Hasunga
anasema Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo
la Japani (JICA), kupitia mradi wa TANRICE2 imetoa mafunzo kwa wakulima
wa mpunga 1,964. Kati ya hao, wakulima 923 wametoka katika skimu za
umwagiliaji za Kimbande Nyasa (Ruvuma), Magoma (Korogwe) Wamiluhindo
(Mvomero), Tulokongwa (Morogoro), SololaNkanga (Sumbawanga) na
Legezamwendo (Tunduru), Litumbadyosi (Mbinga), Njomulole (Namtumbo),
Msanjesi (Namtumbo) na Kyamyorwa (Muleba).
ASDP
II imeandaliwa kwa kuzingatia mikakati yote ya Taifa, ili kukabiliana
na mapungufu na changamoto za sekta ya kilimo na kuongeza kasi ya ukuaji
wa pato la Taifa, kuboresha ukuaji wa pato la wakulima wadogo na kuwa
na uhakika wa usalama wa chakula ifikapo 2025.
Ni
wajibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Wilaya kujenga uwezo
katika huduma za umma ili kuviwezesha vyama vya wakulima wadogo kulima
kibiashara kusaidia kuwaunganisha wafanya biashara wa sekta ya kilimo na
mfumo wa uzalishaji wa wakulima, wafugaji na wavuvi kwa ajili ya soko
na kuendeleza mnyororo wa thamani.
Post A Comment: