Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 16 Mei 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 16 Mei 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo, Dodoma
Serikali
iko katika mchakato wa kufanya ukaguzi na tathmini ya kina ya miradi
yote ya umwagiliaji nchini ili kufanya uhakiki wa eneo la umwagiliaji
kwa lengo la kubaini ubora wa miradi, thamani ya fedha, gharama za mradi
na mahitaji halisi ya sasa ya kuboresha, kuendeleza na kuongeza miradi
mipya ya umwagiliaji.
Aidha,
baada ya tathmini hiyo Serikali itaendelea kutafuta fedha ndani na nje
ya nchi ili kuhakikisha mabwawa na skimu za umwagiliaji nchini ikiwemo
mradi wa umwagiliaji katika bonde la Mkomazi zinaendelezwa na
kuwanufaisha wananchi wa Mombo na taifa kwa ujumla.
Naibu
Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo Bungeni Jijini
Dodoma leo tarehe 16 Mei 2019 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la
Korogwe Vijijini Mhe Timotheo Mnzava aliyetaka kufahamu mpango wa
Serikali katika utekelezaji wa mradi wa Umwagiliaji katika Bonde la mto
Mkomazi.
Alisema
kuwa katika miaka ya 1980 Serikali kupitia washirika wa maendeleo,
Wakala wa Ushirikiano wa Kitalaam wa kimataifa wa Serikali ya Ujerumani (Germany Agency for Technical Cooperation Ltd) ulifanya upembuzi yakinifu (Feasibility studies)kwa
ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Mkomazi
katika tarafa ya Mombo, Halmashauri ya Korogwe. Hata hivyo taarifa za
upembuzi yakinifu na usanifu zilibaini kuwa ujenzi wa bwawa hilo
ungesababisha kuongezeka kwa maji katika ziwa Manga na kupelekea kuzama
kwa Kijiji cha Manga Mikocheni pamoja na mashamba ya wakulima.
Mhe Mgumba alisema kuwa kutokana
na changamoto hiyo katika mwaka 2014/2015, wataalam wa ofisi ya kanda
ya umwagiliaji ya Kilimanjaro walifanya mapitio ya upembuzi yakinifu na
usanifu uliofanywa katika eneo hilo kwa lengo kuepusha uwezekano wa
kufurika kwa Ziwa Manga, kuzama kwa Kijiji cha Manga Mikocheni na
Mashamba ya wakulima kutokana na ujenzi wa bwawa. Mapitio hayo yalibaini
uwezekano wa ujenzi wa bwawa na mradi wa umwagiliaji katika eneo hilo
bila kuathiri wakazi wa eneo hilo. Mapitio ya usanifu huo yalibaini kuwa
ujenzi wa bwawa pekee utagharimu Shilingi 1,543,736,877.
Aidha,
akijibu swali la Mbunge wa Kondoa Mjini Mhe Edwin Mgate Dannda
aliyetaka kufahamu ni lini andiko la mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji
katika Kijiji cha Mongoroma, Kata ya Serya wenye eneo la ekari 3000
utaanza utekelezaji wake, Mhe Mgumba alisema kuwakatika bajeti ya mwaka 2010/2011 Serikali kupitia Idara ya Umwagiliaji ilituma Shilingi
milioni 300 kwa ajili kuendeleza miradi ya umwagiliaji ya Kisese,
Kidoka na Mongoroma Serya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa wakati huo.
Alisema Kati ya fedha hizo Shilingi 143,265,000 zilitumika
kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu katika mradi wa
Mongoroma Serya uliopo katika Kata ya Serya. Kazi zilizofanyika ni
pamoja na upimaji wa sura ya ardhi (Topographical Survey), usanifu wa kina (detail design), matayarisho ya gharama za ujenzi, tathmini ya rasilimali maji (Hydrological survey), tathmini ya awali ya mazingira, utafiti wa udongo (Soil analysis) na masuala ya jamii.
Aliongeza
kuwa Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bwawa la Mongoroma Serya
ulibaini kuwa bwawa hilo lingegharimu Shilingi bilioni 4 kwa wakati huo.
Aidha, bwawa hilo lingekuwa na uwezo wa kumwagilia zaidi ya hekta 3,000
na kunufaisha zaidi ya wakulima12,000 kwa
ajiili ya kilimo cha umwagiliaji, matumizi ya binadamu, unyweshaji wa
mifugo na wanyama pori pamoja na ufugaji wa samaki katika vijiji vya Mongoroma, Serya na Munguri.
Mgumba alisema Serikali
iko katika mchakato wa kufanya tathmini ya kina kwa miradi yote ya
umwagiliaji nchini ili kubaini thamani ya fedha, ubora wa miradi na
mahitaji halisi ya uboreshwaji, uendelezwaji na kuchagua miradi michache
kwa utekelezaji wa ujenzi kwa miradi yenye TIJA, matokeo na manufaa
makubwa kwa wakulima na Taifa kwa ujumla. Aidha, baada ya tathmini hiyo
na kutegemea upatikanaji wa fedha serikali itahakikisha bwawa hilo na
skimu zingine zitajengwa.
MWISHO
Post A Comment: