Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango akisisitiza jambo wakati wa kuagana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) Bi. Maniza Zaman (hayupo pichani), anayehamia nchini Kenya, alipoenda kumuaga Waziri wa Fedha na Mipango ofisini kwake, Jijini Dodoma.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) anayehamia nchini Kenya Bi. Maniza Zaman, akizungumza wakati alipokwenda kumuaga Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango (hayupo pichani), ofisini kwake Jijini Dodoma.
Ujumbe kutoka Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango (wapili kulia), wa kwanza ni Kamisha Msaidizi Idara ya Bajeti Dkt. Charles Mwamwaja, wakati wa kikao cha kuagana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) anayehamia Kenya, Bi. Maniza Zaman, (hayupo pichani).
Na
Josephine Majura, WFM, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amelishauri Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia
Watoto (UNICEF), kuweka namna bora ya kuingiza ajenda ya uwekezaji kwa watoto
katika mikutano mbalimbali inayofanyika
Barani Afrika.
Hayo ameyasema alipokuwa
akiagana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika
la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) Bi. Maniza Zaman, anayehamia nchini Kenya.
Dkt. Mpango alisema Shirika hilo
linatakiwa kuweka mkazo huo ili kuhakikisha nchi za Afrika zinaweka mipango ya
kuwekeza kwa ajili ya watoto kwa kuwa kundi hilo ndiyo Taifa la kesho.
Alisema Serikali ya Tanzania
kwa kutambua umuhimu wa Sekta ya Elimu Nchini, imekuwa ikitoa kipaumbele katika
elimu kwa kutoa elimu ya awali, msingi na sekondari bure kwa lengo la kutoa
nafasi kubwa kwa watoto ili wapate haki yao ya msingi.
Aidha Dkt. Mpango alisema
kuwa katika kuboresha Sekta ya Elimu Duniani ni vema pia masuala ya lishe bora
kwa mtoto yakatiliwa mkazo kwani lishe bora inachangia afanye vizuri dararasani
lakini pia itamsaidia mtoto kuwa na afya bora itakayomfanya aweze kufikiri
vizuri.
“Nitahakikisha agenda za
kulinda haki ya mtoto nchini inapewa kipaumbele kwenye mikutano yetu mikubwa
tunapokuwa tukijadili masuala ya maendeleo kwa ujumla”, alisisitiza Dkt.
Mpango.
Aliongeza kuwa jukumu la
kumlinda mtoto ni la kila mmoja kwakuwa wote walishawahi kuwa watoto hivyo ni
vema kila mmoja atomize jukumu hilo.
Kwa upande wake, Mwakilishi
wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) Tanzania
Bi. Maniza Zaman, anaye hamia nchini
Kenya, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kufanya nae kazi vizuri kwa kipindi
chote alichokaa nchini.
“Tanzania ni nchi nzuri,
watu wake wana upendo, wana utu na wakarimu
karibu kwa mikoa yote 19 hadi 20 niliyowahi kutembelea wakati wa
kutekeleza majukumu yangu”, alisema Bi. Maniza.
Alitoa wito kwa Serikali,
kuendelea kutoa kipaumbele kwa ajili ya Sekta ya Elimu na Afya kwa kuongeza
angalau asilimia moja ya bajeti kila mwaka kwakua zimekuwa na changamoto nyingi
kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya
watu kila siku.
Pia aliiomba Serikali ibuni
mbinu na kuweka mipango endelevu kwa ajili ya watoto itakayowasaidia katika siku zijazo
kwa kuwa takwimu zinaonesha kuwa takriban watoto milioni 2 huzaliwa kila mwaka.
Waziri wa Fedha na Mipango
Dkt. Philip Isdor Mpango alimuahidi aliyekuwa Mwakilishi mkazi wa Shirika la
Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) Bi. Maniza Zaman, kuwa Wizara yake itaendelea
kuhakikisha Sekta hizo zinapata bajeti ya kutosha katika mgawanyo.
Dkt. Mpango amemshukuru kwa
kufanya kazi nchini na kumkaribisha tena na tena hasa kipindi cha mapumziko ambapo
amesema milango ipo wazi muda wowote atakapojisikia kutembelea Tanzania.
MWISHO.
Post A Comment: