Na Ahmed Mahmoud,Longido

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ewor ndeke katika kata ya Kimokokua wilaya ya Longido, Moses Lesikar Leng'ese Ole Nasuaku, anashikiliwa na jeshi la Polisi wilayani humo kwa amri ya Mkuu wa wilaya hiyo akituhumiwa kujipatia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 135 zilizolipwa na wakala wa umeme vijijini Rea kama fidia ya kupisha usambazaji wa umeme.

Akiongea na vyombo vya habari Mkuu wa wilaya hiyo ,Frank Mwaisumbe amesema hatua hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya wananchi wa kijiji hicho wakimtuhumu mwenyekiti wao kujipatia mamilioni ya fedha kupitia mradi wa Rea baada ya kudanganya kuwa maeneo yanayopitiwa na mradi huo ni mali yake wakati si kweli.

Mwaisumbe alifafanua kuwa mwenyekiti huyo alilipwa mara mbili akitumia majina tofauti ,ambapo alilipwa kiasi cha sh,milioni 66 kwa hekari saba na sh,milioni 69 kwa hekari 10 huku akitumia majina ya Lesikar Leng'ese na Moses Leng'ese na kujipatia kiasi hicho cha fedha.

Alisema kuwa kabla ya kutiwa mbaroni kwa mwenyekiti huyo Wanakijiji saba waliohojiwa ,watano walidhibitisha maeneo hayo ni ya kijiji huku wawili ndio walisema ni Mali ya mwenyekiti huyo anayemiliki tangu mwaka 2013 ,ingawa hatua ya upimaji maeneo ya mradi ilishapita tangu mwaka ,2008 .

"Ni kweli tumemkamata kwa kosa la kujipatia fedha kinyume cha SHERIA na kosa hilo ninaangukia kwenye uhujumu uchumi ,nimempa siku saba arejeshe fedha hizo na baada ya hapo tutampeleka mahakamani" Alisema Mwaisumbe

Aliwataja wengine waliotumia mpango huo kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia maeneo hayo ya Kijiji ambao wanatafutwa ni pamoja na Elia Shapashina Kool na Luka Sambeke Ole Mboloso

Wengine ni mwenyekiti wa kitongoji cha Maatiani aliyetambulika kwa jina moja la Kerimboti ,Sindiyo Leakui na Nengolo Sadaka wote wakazi wa Kijiji cha Ewor ndeke.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa fedha hizo zimelipwa wiki tatu zilizopita kama fidia kwa maeneo yaliyopitiwa na mradi huo wa Rea baada ya kupimwa na kuthaminishwa mwaka 2008 ambapo fedha hizo ziliopaswa kuwekwa kwenye akaunti ya Kijiji lakini mwenyekiti huyo na wenzake walitumia akaunti binafsi kujinufaisha.

Wakati mkuu huyo wa wilaya akichukua hatua hiyo wananchi wa Kijiji hicho wakiwemo wanawake wametishia kufunga ofisi ya kijiji hicho kama njia pekee ya kushinikiza kiongozi huyo kuachia ngazi .

Mmoja ya wananchi wa Kijiji hicho, Mbayo Olotito alisema kuwa mwenyekiti wao amekosa uaminifu kwa muda mrefu na wanajipanga kupeleka kilio chao kwa mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo ili kushinikiza kuweza kuchukuliwa hatua zaidi kwa mwenyekiti huyo na wenzake walioshiriki kuhujumu maeneo ya Kijiji na kujinufaisha wenyewe.

"Huyu mwenyekiti kwa muda mrefu amekuwa akichochea migogoro ya Ardhi kwa wananchi na kujinufaisha " Amesema Olo Tito.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: