Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa siku tano wa Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini wakimsikiliza, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua mkutano wao wa siku tano kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza, Machi 18, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisindikizwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe baada ya kufungua Mkutano wa Kazi wa Maafisa Habari na Mwasiliano wa Serikalini kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza, Machi 18, 2019. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela. (picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
PMO 8830 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini wakati alipowasili kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza kufungua mkutano wa Kazi wa Siku Tano wa Maafisa hao , Machi 18, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi , Afisa wa Mawasiliano wa NSSF, Lulu Mengele, Cheti cha Shukuruani kwa udhamini wa NSSF wa Mkutano wa Kazi wa Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini alioufungua kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza, Machi 18, 2019. Kushoto ni Waziri wa Habari ,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi cheti cha shukurani ya udhamini wa Mkutano wa Kazi wa Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Masanja Kadogosa baaada ya kufungua Mkutano wa siku tano wa Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini, Kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza, Machi 18, 2019. Kushoto ni Waziri wa Habari, Umaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
Simu: +255-26-232-2484/232-4560
Mlimwa Kusini,
11 Barabara ya Edward Sokoine,
Nukushi: +255-26-232-1955, S. L. P. 980,
18 Machi, 2019
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU AWATAKA MAAFISA HABARI WAJITATHMINI
WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa amewataka Maafisa Habari,
Uhusiano na Mawasiliano Serikalini wajitathmini kwa kina zaidi kuhusu
namna walivyotekeleza wajibu wao na watafakari njia bora ya kuyatangaza na
kuyatetea mafanikio ya mageuzi makubwa yanayoendelea nchini.
Pia, amewataka Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini
wahakikishe wanatumia vizuri taaluma zao na nyezo wanazopatiwa kusema mambo yanayofanywa
kwenye sekta zote na wasipofanya hivyo watatoa fursa kwa taarifa zinazosemwa na
wapinga maendeleo kuonekana kuwa ni kweli.
Waziri Mkuu ameyasema hayo
leo (Jumatatu, Machi 18, 2019) katika
ufunguzi wa Kikao Kazi cha 15 cha Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini,
kinachofanyika katika ukumbi wa BOT jijini Mwanza. Kikao hicho kinahudhuriwa na
Maafisa Habari na Mawasiliano takbaribani 400.
Amesema maafisa hao
wanatakiwa wakumbuke kuwa wanapaswa kuueleza umma wa Watanzania kwa kina
masuala yanayofanywa na Serikali hususan katika kipindi hiki ambacho Serikali
inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021)
wenye kuweka msisitizo kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda.
“Mkumbuke
kuwa kazi ya utoaji taarifa kwa wananchi kwa sasa si utashi binafsi wa mtoa
habari bali hainabudi kufanywa kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi. Mathalan
Sheria mpya ya Haki ya Kupata Taarifa Na. 12 ya mwaka 2016 yenye kuzitaka
mamlaka za umma kuwapa wananchi taarifa zinazowahusu”.
Waziri Mkuu amesema sheria
hiyo, inakwenda sambamba na sheria nyingine ya kumlinda mwananchi asilishwe
taarifa za uongo, uchochezi na uzushi yaani Sheria ya Huduma za Habari Na. 12
ya mwaka 2016.
Amesema lengo la katiba na
sheria hizo mbili, pamoja na mambo mengine, ni kuwahakikishia wananchi haki ya
kupata habari tena zilizothibitishwa kwa maana ya usahihi wake na kwa wakati. “Sababu
hizo, ndizo zilizofanya niguswe sana na kauli mbiu yenu isemayo: “utoaji habari
sahihi na kwa wakati ni chachu katika kuifikia Tanzania ya kipato cha kati”.
Pia, Waziri Mkuu ametumia
fursa hiyo kupongeza kazi nzuri zinazofanywa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais Ikulu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (hususan Idara yake
ya Habari - MAELEZO) na timu za habari za viongozi wakuu kama Mawaziri, Wakuu
wa Mikoa na watendaji wengine.
Pia, Waziri Mkuu amesema
ameguswa na baadhi ya mada ambazo zitajadiliwa katika kikao kazi hiko, ikiwemo
ya namna ya kushughulikia habari za uongo, kutunga, kughushi na namna kada
yao inavyoweza kusaidia kukidhibiti kichochoro hicho haramu katika habari.
Kadhalika, Waziri Mkuu
amewataka viongozi na watendaji wote wa taasisi za umma, kuanzia sasa washirikiane
na maafisa wa habari kwenye maeneo yao kuhakikisha kuwa habari muhimu kwa
wananchi hazizuiwi kwa urasimu kama hazijazuiwa kisheria. Habari zitolewe kwa
haraka na kwa njia anuai za kisasa.
Waziri Mkuu amemuagiza
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe afuatilie
kuhusu uzinduzi wa tovuti za Halmashauri walioufanya jijini Dodoma tarehe 27
Machi 2017, kama zinafanya kazi ipasavyo.
Amesema lengo la tovuti
hizo ni kuiongezea Serikali uwezo wa kuwapatia wananchi habari na taarifa kwa haraka
kwa kuzingatia kwamba wako katika kipindi muhimu cha mageuzi katika historia ya
nchi, ambapo mambo mengi yanafanyika Serikalini ya kiuchumi na kijamii lakini
hayafikishwi kwa wananchi.
“Kuhusu hili, naiagiza
Wizara ya Habari kufanya tathmini ya mara kwa mara na kuniletea taarifa kuhusu
utekelezaji wa majukumu yenu na matakwa haya ya kisheria miongoni mwa wizara,
taasisi za umma na sekretarieti za mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini”.
Waziri Mkuu amesema
maafisa hao wanapaswa kufahamu kikao chao kimekuja wakati muafaka kwani
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, ipo katika
mwaka wake wa nne wa kutekeleza mageuzi makubwa katika kila sekta zikiwemo za
kiuchumi na kijamii nchini.
Amesema katika kipindi cha
zaidi ya miaka mitatu kazi kubwa tena ya kihistoria imefanywa na Serikali ya
awamu ya tano na wao ni mashahidi wa hayo yanayofanywa. “Ni jukumu lenu sasa
kuuhabarisha umma wa Watanzania kama ambavyo Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania inavyotaka katika Ibara ya 18(d).
Waziri Mkuu ametaja mapinduzi makubwa yaliyofanyika kwenye kila sekta nchini ikiwemo elimu; afya; nishati; mifugo; viwanda; barabara; viwanja vya ndege; uchukuzi wa anga; uchukuzi wa reli; uchukuzi wa majini; madini; sanaa za filamu na muziki; utalii na michezo mbalimbali. Amesema maafisa hao wanapaswa kuyatangaza mageuzi hayo.
(mwisho)
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU,
MACHI 18, 2019.
Post A Comment: