Mkurugenzi wa Fedha na Mipango katika Hospitali ya Rufaa Bugando, jijini Mwanza, Mtawa Suzan Batholomew amefariki dunia baada ya kujirusha kutoka ghorofani muda mfupi baada ya kutoka kusali misa ya saa 12:00 asubuhi leo Jumanne Agosti 28, 2018.
Inaelezwa kuwa mtawa huyo amefariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo, na kupelekea kuumia maeneo ya kiuno na mgongo.
Afisa Uhusiano wa Bugando Lucy Mogele amesema hospitali hiyo haina mamlaka ya kuzungumzia suala hilo na kutaka litafutwe shirika la watawa la Kagera ambalo makao makuu yake yapo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
“Ni kweli Sister Suzan amefariki dunia baada ya kujirusha kutoka ghorofani lakini Bugando hatuna mamlaka ya kuzungumzia suala hilo” alisema Lucy.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza Kamishina Msaidizi wa Polisi Jonathan Shana amethibitisha kutokea kwa tukio na kwamba chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa.
"Bado tupo katika upelelezi kuhusiana na tukio hili,mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando kwa ajili ya uchunguzi na pindi uchunguzi ukikamilika utakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi", alisema.
Aidha ametoa wito kwa wananchi mkoani Mwanza kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi pindi wanapoona wamekwenda kinyume na taratibu za kazi kama vile kujitoa uhai au kujijeruhi kwani ni kosa kisheria.
Habari kutoka hospitalini hapo zinabainisha kuwa katika ofisi aliyokuwa akiifanyia kazi mtawa huyo ambapo yeye alikuwa kiongozi kuna tuhuma za upotevu wa fedha zaidi ya milioni 300 ambazo zilipelekea baadhi ya watumishi wenzake kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi na wengine kufukuzwa kazi.
Post A Comment: