Timu ya taifa ya soka ya wanawake Twiga Stars imetupwa nje ya mashindano
ya kuwania kufuzu fainali za AFCON 2018 kwa wanawake baada kutoa sare
ya 1-1 ugenini dhidi ya Zambia.
Katika mchezo uliomalizika jioni hii Twiga imejitahidi kuzuia kufungwa
lakini imeponzwa na sare ya 3-3 ambayo ilipatikana kwenye mchezo wa
kwanza uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Jumanne
iliyopita.
Zambia sasa imesonga mbele ambapo imebakiza mchezo mmoja itacheza na
mshindi kati ya Namibia na Zimbabwe na endapo itashinda basi itakuwa
imekata tiketi ya kucheza fainali hizo zitakazofanyika nchini Ghana.
Twiga Stars itarejea nyumbani kujipanga tena katika awamu nyingine na
michuano mingine. Tanzania sasa inawakilishwa na Ngorongoro Heroes pekee
ambayo inasubiri kucheza na DR Congo kwenye mchezo wa marudiano baada
ya kutoka 0-0 kwenye mechi ya kwanza.
Post A Comment: