Na Ferdinand Shayo,arusha
Naibu Waziri  Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Antony Mavunde amesema kuwa serikali haitawavumilia Watumishi wa Idara mbalimbali za serikali watakaojihusisha na vitendo vya rushwa na badala yake watachukuliwa hatua kali ili kulinda heshima na taswira ya serikali kwa wananchi .

Mavunde ameyasema hayo wakati akifungua mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika kitaifa jijini Arusha ambapo amewataka Watumishi hao kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu ili kuwapatia huduma bora wananchi na kutatua kero kama ambavyo serikali ya awamu ya tano imekua ikielekeza.

Aidha amewataka Watumishi hao kujipima iwapo wanatimiza wajibu wao kabla ya kudai haki zao kwani hakuna haki inayozidi wajibu vyote viwili vinapaswa kwenda sambamba.

“Serikali inajitaidi kuboresha mazingira ya kazi kwa kuhakikisha kuwa watumishi wanapata stahiki zao kwani kwa sasa serikali imejipanga kulipa madeni ya watumishi na wakandarasi baada ya kumaliza uhakiki wa madeni hayo” Alisema Mavunde

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu ,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Erick Kashinje amesema kuwa chini ya wizara hiyo wameweza kutatua migogoro mingi inayotokea mahali pa kazi na kufikia muafaka kati ya Waairi na Wafanyakazi jambo ambalo linaleta ufanisi katika kazi.

Kashinje amesema kuwa wizara hiyo ina jukumu la kutengeneza ajira pamoja na kuwawezesha vijana na wanawake kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini.

Mjumbe wa Baraza hilo amesema kuwa wamejipanga kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa uadilifu na kuepukana na rushwa ambayo imekua ikizorotesha maendeleo ya nchi
Share To:

msumbanews

Post A Comment: