Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha ameitaka Wizara yake kufanya uchunguzi na kutoa ripoti ya namna ukarabati wa Miundombinu ulivyofanyika katika Chuo cha Ualimu Butimba ili kujiridhisha kama kweli ukarabati huo unaakisi kiasi cha fedha zilizotolewa.
Naibu Waziri Ole Nasha ametoa kauli hiyo Mjini Mwanza baada ya kufanya ziara katika chuo hicho hapo ambapo amesema hajaridhishwa na ukarabati ulivyofanyika kwa kuwa Chuo hicho kilipatiwa kiasi cha takribani Milioni Mia Nane Sitini na Tatu.
Ole Nasha amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha Vyuo vya Ualimu vinakuwa na mazingira mazuri ya kuwaandaa Walimu wanaokwenda kufundisha katika shule mbalimbali hapa nchini hivyo ni jukumu la Wakuu wa Taasisi na Vyuo vya Elimu kuhakikisha wanasimaia Miradi mbalimbali ya Elimu kwa ukamilifu na kuwa Serikali haitasita kuchua hatua kwa yeyote atakayeshindwa kusimamia Miradi hiyo kwa weledi.
“Chuo hiki kimepatiwa takribani Milioni Mia Nane Sitini na Tatu kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu kama hivi ndivyo ukarabati uliofanyika hauonyeshi thamani ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya Chuo hiki cha Ualimu Butimba, kwa kweli Sijaridhishwa”alisisitiza Naibu Waziri huyo.
Akitoa maelezo Mkuu wa Chuo hicho John Ole Meiludie amejitetea kuwa kazi hiyo ya ukarabati imefanyika kwa umakini isipokuwa wanafunzi wenyewe ndiyo wanachana nyavu za madirisha lakini pia hali ya mvua zinaponyesha huondoa rangi ambayo inakuwa imepakwa katika majengo ya Chuo hicho.
Akiwa Mkoani Mwanza Naibu Waziri Ole Nasha ametembelea Shule ya Sekondari Nyegezi iliyoko Wilaya ya Nyamagana na Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma VETA kilichopo wilaya ya Ilemela na kuridhishwa na namna walivyotekeleza miradi ya Elimu.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
05/03/2018
Post A Comment: