Siku tatu baada ya Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu kupanda jukwaani kumnadi mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Siha, Dk Godwin Mollel, Chadema imesema itamfikisha katika kamati ya maadili kama ilivyoshauriwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Mkuu huyo wa wilaya alipanda jukwaani Januari 21 katika uzinduzi wa kampeni za Dk Mollel katika viwanja vya KKKT Karansi, huku akisema Serikali haijaribiwi hivyo ni vyema kila mmoja akahakikisha anadumisha amani na kufanya siasa za kistaarabu kipindi chote cha kampeni.
Baada ya kauli yake hiyo, Mwananchi lilizungumza na mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima na kubainisha kuwa mkuu huyo wa wilaya hakufanya jambo sahihi.
Kailima alisema vyama vinavyoshiriki uchaguzi katika jimbo hilo ndio vyenye jukumu la kumshtaki katika kamati ya maadili inayoundwa na wajumbe wa vyama hivyo katika jimbo husika na kwamba, jambo hilo linapaswa kufanyika ndani ya saa 72, tangu apande jukwaani.
Akizungumzia mchakato wa kumshtaki Buswelu, mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema watawasilisha malalamiko yao yenye hoja tano.
Kwa mujibu wa Kailima, kama kuna uvunjifu wa maadili, kamati hiyo ina mamlaka ya kuwasilisha hilo katika ngazi nyingine ya kisheria kama polisi au kwa mkurugenzi wa mashtaka (DPP).
Uchaguzi wa Siha na Kinondoni unaovihusisha vyama 12 utafanyika Februari 17, huku ukitajwa kuwa ni mpambano mkali baina ya CCM na Chadema.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya waliokuwa wabunge; Mollel (Siha-Chadema) na Maulid Mtulia (Kinondoni-CUF) kujivua uanachama wa vyama hivyo kwa maelezo kuwa wanamuunga mkono Rais John Magufuli na baadaye kujiunga CCM. CCM imempitisha Mtulia kugombea Kinondoni na Mollel (Siha), huku Chadema ikimsimamisha naibu katibu mkuu wake (Zanzibar), Salum Mwalimu (Kinondoni) na Elvis Mosi (Siha).
Share To:

msumbanews

Post A Comment: