Mwenyekiti wa Bunge,  Mussa Zungu amemuomba radhi kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kwa kushindwa kutambua mchango wake kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
Hatua hiyo imefutia mwongozo ulioombwa na wabunge wawili Chadema, kuwa mchango wa Mbowe haukutambulika licha ya kufika Bukoba, kutoa misaada na kushirikiana na waathirika wa tukio hilo hadi sasa.

Aliyeanza kuomba mwongozo ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche ambaye alihoji kwa nini mwenyekiti huyo wa Bunge amewatambua viongozi waliofika eneo la tukio na kutoa misaada lakini ameshindwa kumtambua Mbowe ambaye mpaka sasa yupo eneo la tukio na ametoa msaada.

Mbunge mwingine ni Pascal Haonga wa Mbozi ambaye alisema Mbowe ni kiongozi mkubwa na halitakuwa jambo la maana kama mchango wake hautatambulika kwani suala hilo siyo la kisiasa.

Kufuatia mwongozo huo, Zungu aliomba radhi na kuongeza kuwa anamtambua Mbowe kama kiongozi aliyetoa msaada kwa waathirika hao.

Awali, Mwenyekiti huyo wa Bunge baada ya kuingia ukumbini alitoa pole kwa waathirika wa tetemeko hilo lililoua watu 17 na kuwatambua watu waliochangia tukio hilo akiwamo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na wafanyabiashara.  Baada ya kipindi cha maswali na majibu kuisha, mwenyekiti huyo aliwatambua wafanyabiashara wengine waliotoa msaada kwa waathirika hao lakini hakugusia msaada ulitolewa na Mbowe.

www.msumbanews.blogspot.com

 

Share To:

msumbanews

Post A Comment: