Wahitimu wa Chuo cha Ualimu Korogwe wakiwa kwenye mahafali ya 62 ya Chuo hicho (Picha na Yusuph Mussa)
MENEJA wa Benki ya NMB Tawi la Korogwe Mwampeta Lugano akizungumza kwenye mahafali ya 62 ya Chuo hicho (Yusuph Mussa)
MKUU wa Chuo cha Ualimu Korogwe Hassan Ismail akizungumza wakati wa maafali ya 62 ya Chuo cha Ualimu Korogwe kama mgeni rasmi(Picha na Yusuph Mussa)CHUO
cha Ualimu Korogwe, pamoja na kutoa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA), lakini chuo hicho hakina huduma ya internet, hivyo
kuwafanya wanafunzi wanaojifunza kozi hiyo kuwa ngumu wakati wa kufanya
kwa vitendo.
Lakini pia,
pamoja na Serikali kujenga maktaba ya kisasa kwenye chuo hicho yenye
thamani ya zaidi ya sh. milioni 250, lakini imeshindwa kuweka mtandao wa
internet, sababu maabara hiyo pia ina kompyuta kwa ajili ya kujisomea.
Hayo
yalisemwa mwishoni mwa wiki na wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Korogwe
kwenye risala iliyosomwa na Izadine Masanga kwenye mahafali ya 62 ya
chuo hicho kikongwe nchini, ambapo wanachuo 724 walihitimu mafunzo ya
stashahada maalumu ya ualimu ya sayansi, hisabati na TEHAMA kwa shule za
sekondari.
"Pamoja
na mafunzo ya TEHAMA kutolewa chuoni, maabara ya TEHAMA ni ndogo sana
na haina vifaa vya kutosha kulingana na idadi ya wanachuo. Kwa mfano,
upatikanaji wa vifaa kama vinukushi, printer na vingine vinavyokosekana,
vinasababisha changamoto kubwa sana wakati wa kufanya mafunzo kwa
vitendo (practical). Pia kukosa Mkongo wa Taifa.
"Maktaba
mpya kubwa na ya kisasa kukosa mfumo wa internet pamoja na vitabu
muhimu vyenye kukidhi haja katika masomo ya ngazi mbalimbali. Maombi
yetu, tunaomba kuongezewa samani hususani meza na viti kwa matumizi ya
wakufunzi na wanachuo madarasani, na kuwekwa mfumo wa internet hususani
maeneo ya maktaba mpya na maabara ya ICT" ilisema risala hiyo.
Mkuu
wa Chuo hicho Hassan Ismail alisema moja ya changamoto chuoni hapo ni
kukosa uzio, ambapo karibu eneo lote la chuo lipo wazi, na hiyo kutoa
nafasi kwa wanajamii wanaokizunguka chuo kufanya njia karibu maeneo yote
ya chuo pamoja na kuchungia mifugo yao
Ismail
alisema, pamoja na chuo hicho kutoa mafunzo ya sayansi, hisabati na
TEHAMA, lakini maabara yake haina mtandao wa internet, huku kompyuta
zilizopo kushindwa kukidhi mahitaji ya chuo hicho ambacho kinachukua
wanachuo 1,200 kwa wakati mmoja, ambapo kwa sasa wapo wanachuo 1,051.
Alisema
changamoto nyingine ni upungufu wa samani katika ofisi za wakufunzi na
madarasani, upungufu wa vitabu vya masomo ya sayansi, hisabati na TEHAMA
katika maktaba ya chuo, na uchakavu wa nyumba za watumishi.
Mgeni
rasmi kwenye mahafali hayo, Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Korogwe
Lugano Mwampeta alisema katika kupunguza changamoto ya chuo hicho, benki
ya NMB itatoa viti na meza vyenye thamani ya sh. milioni tano.
MWISHO.
Post A Comment: