Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa wa Mapambano dhidi ya UVIKO -19 imetenga shilingi bilioni 1.01 kwa ajili ya mafunzo ya kuwajengea uwezo waongoza watalii wanawake takribani 1060 nchini. Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mary Masanja (Mb) wakati wa kuhitimisha mafunzo ya waongoza watalii wanawake 89 yaliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. “Mafunzo haya ni mahususi kwa wanawake kama jitihada za makusudi kabisa za Serikali kuhakikisha kuwa wanawake wanapata fursa za kuchangia katika maendeleo ya nchi kupitia utalii na kunufaika kupitia sekta hiyo” ” amefafanua Masanja. Amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri kwa kuitangaza vyema Tanzania ndani na nje ya nchi. “Natambua mmekuwa mabalozi muhimu mnaotegemewa kuiuza nchi yetu hivyo sifa ya kwanza mnayotakiwa kuwa nayo ni uzalendo. Wageni mnaowapokea wana sifa mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa hivyo wakati mnatekeleza majukumu yenu mnapaswa kuwa na uelewa mpana wa shughuli za utalii na pia muwe na maadili, weledi na uadilifu”amesema Masanja. Aidha, amewaasa waongoza watalii hao kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa watalii wanapowasili nchini ili kujenga taswira nzuri ya Tanzania na kumfanya mtalii aweze kurudi. Naye, Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori (MWEKA), Prof. Jafari Kideghesho amesema kuwa mafunzo hayo yatawaongezea washiriki uwezo na kujiamini zaidi katika kufanya shughuli za waongoza watalii ambazo kwa sehemu kubwa zimekuwa zikitekelezwa na wanaume. Amesema ongezeko la wanawake katika kada ya waongoza watalii itaongeza idadi ya watalii hasa kwa kuwa wanawake wanaaminika na kupendwa zaidi kutokana na hulka yao ya upole, ukarimu na uadilifu Mafunzo kwa waongoza watalii wa kike yanasimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori (MWEKA) na mada zilizotolewa kwa washiriki ni usimamizi wa utalii, kanuni na maadili za waongoza watalii, ukarimu,ikolojia namna bora ya mawasiliano,tafsiri ya rasilimali mbalimbali za watalii , mikakati ya kukabiliana na majanga
Share To:

Arusha Newsroom

Post A Comment: