Mratibu wa kitaifa programu ya kuzuia na kukabiliana na Upungufu wa Vitamini A nchini kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Francis Modaha, akimkabidhi Mganga mkuu wa Serikali kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.Aifillo Sichalwe Chupa ya Kitakasa Mikono ikiwa ni ishara ya kumkabidhi vifaa vya kupambana na UVIKO-19 kutoka Shirika la Kimataifa la Nutrition International kwa ajili ya watoa huduma za afya katika mikoa 12 nchini na mikoa Mitano ya Zanzibar.

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifillo Sichalwe akikabidhi boksi la Barakoa kwa Mkurugenzi wa huduma za Afya Mwanahamisi Hassan kwa niaba ya Ofisi ya Rais –TAMISEMI ikiwa ni ishara ya kupokea vifaa vya kuwakinga na UVIKO-19 watoa huduma za afya katika mikoa 12 nchini vilivyotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa niaba ya Shirika la Nutrition International.


Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifillo Sichalwe akikabidhi boksi la Kitakasa Mkono kwa Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mohamed Abdulla kwa ajili ya Mikoa 5 ya Zanzibar ikiwa ni ikiwa ni ishara ya kupokea vifaa vya kuwakinga na UVIKO-19 watoa huduma za afya wakati wa huduma za Mwezi wa afya na Lishe ya Watoto. Mkurugenzi wa huduma za Afya- TAMISEMI Mwanahamisi Hassan akimkabidhi kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Dkt Samuel Seseja boksi la Barakoa ikiwa ni ishara ya kupokea vifaa vya kuwakinga na UVIKO-19 kwa niaba ya Wganga Wakuu wa Mikoa 12 nchini, ambayo itapatiwa vifaa hivyo.

******************************

Na, Jackson Monela -Dodoma

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekabidhi vifaa vya kujikinga na UVIKO-19 kwa Mikoa 12 ya Tanzania Bara na 5 ya Zanzibar vilivyotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kupitia shirika la Kimataifa la Nutrition International (NI) ikiwa ni kuwakinga watoa huduma ya afya hususani katika zoezi la Utoaji wa Matone ya Vitamini A nchini.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa wawakilishi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira Mganga Mkuu wa Serikali Dkt Aifillo Sichalwe amesema vifaa hivyo vitaenda kuwasaidia watoa huduma za afya walio mstari wa mbele katika kutoa huduma za afya nchini bila kuwasahau watoa huduma za afya ngazi ya jamii (CHW)

Dkt Sichalwe amesema kutokana na changamoto ya UVIKO-19 Serikali inaendelea kuwapatia vifaa vya kujikinga na maambukiz ya UVIKO-19 watoa huduma waliopo katika vituo vya afya ili kuwawezesha kuendelea kutoa huduma za afya kwa ufanisi ikiwemo Kampeni ya utoaji wa Matone ya Vitamini A inayofahimika kama Huduma ya Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto.

“Vifaa hivi vimeanza kutolewa katika mikoa 12 ya Dodoma, Geita, Kagera, Morogoro, Katavi, Mwanza, Kilimanjaro, Shinyanga, Simiyu, Singida, Tabora na Tanga pamoja na Mikoa yote mitano ya Tanzania Visiwani na mikoa hii imeteuliwa kwa sababu ilikuwa na ufanisi duni katika utoaji wa huduma za mwezi wa afya, hivyo kupitia msaada huu utasaidia kuimarisha kiwango cha katika utoaji wa huduma za matone ya Vitamini A kwa watoto wengi zaidi” Alisema Dkt.Sichalwe.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Ray Masumo ameishukuru Serikali ya Cananda kupitia Shirika lake la Nutrition International (NI) kwa kuendelea kuiunga mkono serikali katika vita dhidi ya UVIKO-19 na changamoto nyingine za Kilishe.

Dkt. Masumo amesema vifaa hivi vitawasaidia watoa huduma ya afya waliopo mstari wa mbele katika kutoa huduma za afya ikiwemo Huduma ya mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto kwani malengo yaliyopo ni kuhakikisha ifikapo Mwaka 2025 watoto wote nchini wafikiwe na huduma ya matone ya Vitamini A kupitia vituo vya afya vilivyopo nchini.

Nae Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Nutrition International (NI) Dkt Daniel Nyagawa amesema wamechukua uamuzi wa kutoa vifaa kwa Serikali ikiwa kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazochukuliwa katika kupambana na UVIKO-19 na wataendelea kushirikiana na katika afua nyingine ikiwemo zile za Kilishe ambazo shirika hilo limekuwa likizitekeleza hapa nchini.

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mkurugenzi wa huduma za Afya Dkt.Mwanahamisi Hassan amesema vifaa hivyo vitawasaidia watoa huduma za afya waliopo mstari mbele katika vita ya UVIKO-19 hivyo anawakaribisha wadau wengine kujitokeza katika kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na serikali katika vita hiyo.

Jumla ya Katoni 6000 za Barakoa (Mask) na Vitakasa Mikono (Sanitizer) lita 6000 vyenye gharama ya Milioni 57 vimetolewa na vitasambazwa katika mikoa 17 ikiwemo 12 ya Tanzania bara na 5 ya Tanzania visiwani.

Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: