WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi na watendaji wanaosimamia miradi ya ujenzi waongeze kasi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuwapa fursa wananchi wafaidi matunda ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar. 

 

Ametoa wito huo leo mchana (Jumapili, Januari 9, 2022) wakati akizungumza na mamia wa wakazi wa Jimbo la Kiwani, Mkoa wa Kusini Pemba mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha afya cha shehia ya Kendwa ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za sherehe ya miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar. 

 

"Nitumie fursa hii kuwaomba viongozi na watendaji wanaosimamia mradi huu waendelee kushirikiana na kufanya kazi kwa kasi zaidi ili kukamilisha ujenzi huu kwa wakati uliopangwa ili kuwapa fursa wananchi wafaidi matunda ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar."


“Nilipofika, nimekagua majengo kwenye zote kuanzia chini hadi juu. "Naipongeza kamati ya usimamizi wa ujenzi wa kituo hiki kwa kusimamia vizuri ujenzi wa kituo hiki. Ninaziagiza Kamati nyingine hapa nchini, ziige mfano wa Kamati hii ya Kendwa. Niliposikia fedha iliyotumika sikuamini. Fedha kidogo lakini imetoa majengo mazuri yenye viwango."

 

Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho, Msimamizi Mkuu wa Majengo kutoka ZBA, Mhandisi Said Malik Said alisema ujenzi wa kituo hicho unaofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ulianza Agosti 28, mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Februari 27, mwaka huu.

 

"Gharama za ujenzi ni shilingi milioni 388 lakini hadi sasa zimetumika shilingi milioni 270. Kitakapokamilika, kituo kitakuwa na majengo ya OPD, maabara, chumba cha daktari, vyoo, chumba cha kumfanyia mgonjwa uchunguzi wa awali, chumba cha sindano na kufunga vidonda, kitengo cha meno, wodi ya akinamama wajawazito na nyumba ya daktari yenye uwezo wa kuchukua watumishi wawili kwa pamoja (2-in-1).

Share To:

Post A Comment: