Na Rhoda Simba, Dodoma
WANANCHI wametakiwa kulipia kodi 
ya pango la Ardhi kabla ya Januari mosi mwaka huu ili kuepuka riba ya asilimia
moja ambayo watatozwa kila mwezi kama faini endapo  watachelewa kulipa
kodi hiyo.
Hayo yamesemwa leo Disemba 30 jijini
hapa na Kamishina wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi,Nathaniel Nhonge wakati  akizungumza na waandishi wa habari
kuhusiana na kodi ya  pango hilo la Ardhi.
Aidha Nhonge amesema Wizara hiyo imeweka
utaratibu mzuri  ili kuhakikisha wanatoa huduma bora za ulipaji kodi
ambapo wameanzisha kituo cha mawasiliano kwa wateja na  wanaweza
kuwahudumia wananchi popote walipo ili kuwawezesha kulipa kodi.
“Badala ya kutumia muda mwingi kupanga
foleni tumeona ni bora kuanzisha huduma hiyo kwa wateja ili waweze kupata
huduma za malalamiko yao popote walipo”amesema Nhonge
Nhonge amesema  mikakati
ya Wizara hiyo  ni kuhakikisha ina pima ardhi kwa kasi ili kila mtanzania
aweze kumiliki ardhi ambapo tayari Wizara hiyo ilishapokea fedha kiasi 
cha Shilingi bilioni 50 kutoka Serikalini.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Kodi
Wizara ya Ardhi,Nyumba na maendeleo ya Makazi Denis Masami amesema kuwa katika
kipindi cha kuelekea mwisho wa mwezi muitikio wa ulipaji kodi ya pango la ardhi
umeongezeka ambapo hadi sasa wameshakusanya kiasi cha Shilingi bilioni 60 na
malengo ni kukusanya bilioni 221.
“ kwa wiki moja tunakusanya bilioni 3 hadi 4 na hapa tunaona jinsi gani wananchi walivyokuwa na muitiko katika ukusanyaji wa kodi hii ya pango matarajio yetu ni kila mwananchi anayemiliki ardhi alipe kodi ya pango”amesema Masami
MWISHO.
 
Post A Comment: