**************************

NA MUSSA YUSUPH,MISSENYI

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Christina Mndeme, ameagiza kupimwa kwa maeneo yote yanayotekelezwa miradi ya ujenzi wa shule, hospitali, zahanati na vituo vya afya kwa dhumuni la kuzuia uvamizi na migogoro ya ardhi.

Naibu Katibu Mkuu Bara, alitoa agizo hilo wilayani Missenyi, Mkoa wa Kagera wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Bulembo, alipokwenda kukagua ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo.

“Maeneo yote yanayojengwa shule na hospitali yapimwe kisha yapatiwe hati miliki kuzuia migogoro ya ardhi. Lakini pia wananchi washiriki kuhakikisha maeneo haya hayavamiwi,” alisisitiza.

Akikagua majengo ya hospitali hiyo huku mvua ikinyesha, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, aliwahakikishia wananchi wa wilaya hiyo kwamba baada ya ujenzi wa hospitali kukamilika, serikali italeta wataalamu wa kutosha kutoa huduma kwa wananchi.

“Hapa tusikose daktari bingwa wa akina mama na watoto, tutakuwa na dirisha maalum la wazee, tutakuwa na gari maalum la wagonjwa na ndio maana nimeagiza barabara inayoingia hospitalini itengenezwe kwa kiwango cha lami,” alieleza.

Alisisitiza kuwa: “Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za ziada sh. milioni 300 kujenga jengo la idara ya dharura, lakini kama hakuna miundombinu mizuri ya barabara hilo haliwezekani. Mhandisi hakikisha barabara inajengwa.”

Alibainisha kuwa serikali inajenga miundombinu ya elimu na afya kwa lengo la kuondoa kero kwa wananchi kwa sababu afya ndio msingi namba moja kwa binaadamu.

Aidha, aliagiza baada ya hospitali kukamilika huduma za uzazi zianze na serikali italeta vitanda vya kujifungulia na uwepo wa dawa za kutosha.

Hata hivyo, alimuagiza fundi mkuu anayejenga hospitali hiyo ya wilaya kuharakisha ujenzi kwani ifikapo Desemba mwaka huu, huduma zianze kutolewa kwa wananchi.

“Nasisitiza hospitali itakapokamilika, tulete watumishi wenye maadili na uwajibikaji wa kuwahudumia,” alieleza.

Aliwaomba wananchi pindi watakapoona utekelezaji wa Ilani ya CCM unasuasua watoe taarifa ili hatua zichukuliwe kwa wahusika.

Akizungumzia sababu za mradi huo kuwa nyuma ya utekelezaji kwa wiki tatu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Waziri Kombo, alisema mradi huo ulichelewa kwa sababu ya mvua na ukosefu wa vifaa ndani ya wilaya hiyo.

Alisema mafundi wanalazimika kusubiri tofali kukauka ili waendelee na ujenzi kwa sababu ya mvua, hivyo kusababisha kuchelewa kwa mradi huo.

Kuhusu ukosefu wa vifaa vya ujenzi ndani ya wilaya hiyo, alieleza kuwa hali hiyo imesababishwa na wingi wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi ndani ya wilaya, hivyo wanalazimika baadhi ya vifaa kuagiza Arusha na Dar es Salaam.

Mbunge wa Jimbo la Nkenge (CCM) Frolence Kyombo, aliishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kutoa fedha za ujenzi wa hospitali hiyo ambayo itatatua changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: