Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara hiyo leo Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara hiyo leo Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu (katikati) akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara hiyo leo Jijini Dar es Salaam.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

**************************

NA EMMANUEL MBATILO,DAR ES SALAAM

Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) imeridhia kurudisha mfumo wa ukusanyaji Ushuru wa Maegesho kwa njia ya kielektroniki (TeRMIS) uanze kutumika tena kuanzia tarehe 1 Desemba, 2021 katika maeneo yote ambapo mfumo huo umefika.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa hadi sasa TARURA kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI tayari wamezifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji ushuru wa maegesho ambapo ilikuwa changamoto kwa watumiaji.

"Ukusanyaji wa Ushuru wa Maegesho ya magari kwa kutumia mfumo wa TerMIS utapunguza mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali na kuwezesha fedha hizo kuingia moja kwa moja Serikalini. Kutokana na umuhimu wake ninarejesja matumizi ya Mfumo huu kuanzia tarehe 1 Desemba 2021". Amesema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy amesema miongoni mwa changamoto ambazo wamezifanyia kazi ni pamoja na Wateja kutopatiwa taarifa za kudaiwa ushuru wa maegesho kwa wakati, Kiwango kikubwa cha gharama za maegesho, Muda wa kulipa ambapo hapo awali mtumiaji wa maegesho alitakiwa kulipa ushuru ndani ya siku 7 tangu alipotumia maegesho na endapo atashindwa kulipa ndani ya muda huo alipaswa kulipa mara mbili ya ushuru aliokuwa anadaiwa. Na endapo atazidisha siku 14 pia alitakiwa Ushuru wa Maegesho pamoja na faini ya shilingi 30,000.

"Mtumiaji wa maegesho sasa atatakiwa kulipa ushuru ndani ya siku 14 badala ya siku 7 tangu alipotumia maegesho na endapo atashindwa kulipa ndani ya muda huo atatakiwa kulipa Ushuru wa Maegesho pamoja na faini ya shilingi 10,000 badala ya shilingi 30,000 zilizokuwa zikitozwa awali. Hivyo adhabu wa shilingi 30,000/- nimeifuta". Amesema

Pamoja na hayo ameitaka TARURA kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi hasa kwa Mikoa ilioanza kutumia mfumo huo ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanza, Singida, Iringa na Dodoma ili kuwepo na uelewa wa kutosha kabla ya kuanza tena kwa matumizi ya mfumo huo.

Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: