Mbunge wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Aysharose Mattembe (katikati) akigawa mbegu bora za alizeti kwa Vikundi mbalimbali vya Wanawake mkoani Singida jana, ikiwa ni mwendelezo wa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha kilimo cha zao hilo.

Mbunge wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Aysharose Mattembe (kuliai) akigawa mbegu bora za alizeti kwa Vikundi mbalimbali vya Wanawake mkoani Singida jana..
Zoezi la ugawaji mbegu likiendelea.
Mbegu zikipokelewa.
Vikundi mbalimbali vya akimama Wilaya ya Singida mjini wakionyesha mifuko ya mbegu bora za alizeti muda mfupi baada ya kukabidhiwa na Mbunge Mattembe.
Katibu wa CCM Wilaya ya Singida Mjini Shaban Karage akikabidhi baadhi ya mifuko ya mbegu hizo kwa wanawake wa wilaya hiyo kwa niaba ya Mbunge.
Baadhi ya Wanawake wakitazama mbegu hizo wakati wa zoezi la makabidhiano.

Mbunge Mattembe akizungumza kwenye tukio hilo, kushoto ni Katibu wa CCM Mkoa wa Singida Lucy Shee.

Zoezi likiendelea.
Mbunge akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wanawake wa Mkoa wa Singida 
Ugawaji wa mbegu ukiendelea.
Mbunge akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wanawake wa Mkoa wa Singida. 
 


Na Godwin Myovela, Singida


MBUNGE wa Viti Maalum CCM Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe amekabidhi msaada wa mbegu bora za kisasa za alizeti zaidi ya Tani 10 zenye thamani ya shilingi milioni 35 kwa Vikundi vya Wanawake wa mkoa wa Singida-ikiwa ni mwendelezo wa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuongeza tija ya kilimo cha zao hilo.

Mattembe akiwa kwenye ziara ya kuhamasisha tija ya kilimo hicho sambamba na kugawa mbegu hizo kwa nyakati tofauti ndani ya wilaya za Mkalama, Manyoni, Iramba, Ikungi, Wilaya ya Singida na Singida Manispaa, pia aliwataka wanawake kutobweteka na badala yake kila mmoja kujipanga ipasavyo kwa kuhakikisha anatumia fursa mbalimbali zitokanazo na kilimo katika kujikwamua na umasikini.

Zoezi hilo liliambatana na mafunzo kutoka kwa wataalamu mbalimbali wa kilimo juu ya namna bora ya kumwezesha mkulima kuongeza tija na uzalishaji wa zao la alizeti katika muktadha chanya wa kuongeza kipato cha mtu mmoja, sanjari na kuchagiza ongezeko la uzalishaji wa mafuta ya kula nchini kwa azma ya kupunguza gharama kubwa za takribani bilioni 474 ambazo hutumiwa na serikali kila mwaka kuagiza mafuta hayo kutoka nje.

Wakizungumza baada ya tukio hilo, baadhi ya wanawake mbali ya kumpongeza Mattembe, waliahidi kutumia mafunzo na mbegu hizo katika kuhakikisha wanajiimarisha kiuchumi-kwa mantiki ya matumizi ya kila kilo 6 za mbegu zilizotolewa na Mbunge huyo kwa kila mwanamke sasa ni dhahiri baada ya mavuno zinakwenda kuzalisha zaidi ya gunia 36 ambazo ni wastani wa fedha zaidi ya milioni 2.5.

“Kilo mbili za mbegu hiyo ya alizeti kama zitapandwa kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo huzalisha kati ya gunia 12 hadi 16, hivyo kwa idadi ya kilo 6 zilizotolewa na Mattembe kwa kila mmoja wetu zinakwenda kuzalisha magunia 36 ambayo bei ya soko kwa sasa ni zaidi ya milioni mbili,” alisema mmoja wa wanawake hao ambaye pia ni Diwani Viti Maalum Singida Mjini, Margaret Malecela.

Mjumbe wa Baraza la Umoja wa Wanawake Wilaya ya Singida Mjini na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, Shaban Karage, alisema mbali ya msaada wa mbegu hizo katika nyanja ya kilimo, kumekuwa na jitihada za makusudi za Mbunge Matembe katika kuleta hamasa na  ustawi kwenye maeneo mengine mbalimbali ya kijamii ikiwemo afya, elimu na ujasiriamali.

Karage alisema ameridhishwa na Mattembe na wabunge wenzake wa mkoa wa Singida kwa namna wanavyotekeleza kwa vitendo maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan na Ilani ya CCM juu ya dhamira na takwa la uwajibikaji wa viongozi kwa masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo na ustawi wa watu.

“Ni mattembe huyu huyu aliyetupatia gari la wagonjwa ‘ambulance,’ mashuka na vitanda vya wagojwa,  pia ni Mattembe huyu huyu aliyetupatia mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na vifaa vya TEHAMA kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo pale shule ya Sekondari Mwanamwema na mengine mengi. Leo sote tunashuhudia namna alivyojitoa kwa dhati kwenye eneo la kilimo,tunamshukuru sana kwa moyo wake,” alisema Karage.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: