NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi ametoa Siku 14 kwa Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuhakisha kuwa anafamy uhakiki wa madeni yote ya watumishi na kuyawasilisha Ofisi ya Rais Utumishi ili waweze kulipwa haki yao wanayoistahili.

Ndejembi ametoa agizo hilo alipofanya ziara katika Manispaa hiyo kwa ajili ya kuzungumza na watumishi wa umma lengo likiwa kuwasikiliza changamoto zao na kuzitatua papo kwa papo.

Akijibu changamoto hiyo ya malimbikizo ya mishahara ambayo wanadai watumishi hao, Naibu Waziri Ndejembi amesema Wizara ya Utumishi imekua ikilipa madeni hayo kwa haraka pindi ambapo wamekua wakiletewa orodha ya watumishi wanaodai na kwamba watumishi wanapoona wamechelewa kulipwa wajue shida haipo wizarani bali ipo kwa Maafisa Utumishi kwani wao ndio wamekua wakichelewesha upelekaji wa majina.

"Natoa siku 14 mpaka ifikapo Oktoba 22 Afisa Utumishi wa Manispaa ya Songea na wengine wote nchini sisi Ofisi ya Rais Utumishi tuwe tumepata madeni ya watumishi wote wa Manispaa ya Songea wanaostahili kulipwa ili tuweze kuyafanyia uhakiki yaweze kurudishwa,Sisi Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inajali watumishi wake hivyo tuleteeni majina tuyahakiki na kuyapeleka Hazina ili waweze kulipwa wote haki yao.

Maafisa Utumishi harakisheni kufanya uhakiki na kutuletea orodha hizo, hizi ni haki za watumishi wetu siyo hisani ni jasho lao hivyo wanapaswa kulipwa stahiki zao, na nitoe wito pia Kwa Watumishi wote wenye kudai fuatilieni majina yenu kwa Maafisa Utumishi ili ndani ya hizo wiki mbili nilizotoa tuweze kupata orodha yenu na kuifanyia kazi," Amesema Naibu Waziri Ndejembi.

Akijibu changamoto ya watumishi wa umma waliopandishwa madaraja mwaka 2016 hadi 2017 na kisha baadaye kuondolewa madaraja hayo, Naibu Waziri Ndejembi amesema hakuna mtumishi wa umma aliyepanda daraja kwa kipindi hicho kwani baadaye walitumiwa tena barua za kufuta madaraja hayo.

"Naomba ieleweke baada ya kutumiwa barua za kupandishwa madaraja katika kipindi hicho cha 2016 na 2017 baadaye walitumiwa tena barua za kufuta madaraja hayo kwa kuwa Serikali ilihitaji kufanya uhakiki lakini baada ya uhakiki Novemba 2017 tulianza kupandisha tena madaraja hivyo niwaombe mtambue hakuna daraja linaloitwa Daraja la Mei 2016 lilishaondolewa kwa agizo la Serikali.

Katika kutambua umuhimu wa watumishi wetu wa umma bajeti ya upandishaji madaraja kwa watumishi mwaka huu ilikua tupandishe watumishi 91,000 tu lakini kwa upendo wa Rais Samia kwenu watumishi alitoa maelekezo kuwa tupandishe yeyote ambaye anastahili kupanda daraja mwaka huu na hivyo tumepandisha mpaka Sasa 174,000 hivyo tumekwenda mara mbili ya bajeti iliyokua imepangwa, tumpongeze Rais wetu," Amesema Ndejembi.

Naibu Waziri Ndejembi pia ametoa wito kwa Watumishi wa umma nchini kuchukua tahadhari za ugonjwa wa UVIKO-19 ikiwa ni pamoja na kuchoma chanjo kama ambavyo Rais Samia amekua akishauri na kuwataka kuwa mstari wa mbele kuwaelimisha wananchi madhara ya ugonjwa huo na kuwashauri kujitokeza kwa wingi kuchoma chanjo ili kuweza kujikinga na ugonjwa huo.

 
 




 
Share To:

Post A Comment: