Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Viongozi na Watendaji watakaosimamia utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika leo jijini Arusha.

Baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Arusha watakaotekeleza Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati akizindua Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania leo jijini Arusha.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiteta na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella wakati wa uzinduzi wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania uliofanyika leo jijini Arusha.


Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzindua Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania leo jijini Arusha.


Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga akielezea lengo la Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania uliozinduliwa leo jijini Arusha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Watendaji watakaosimamia utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania mara baada ya kunduzia mradi huo leo jijini Arusha.


Na. Nasra H. Mondwe-Arusha


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Viongozi na Watendaji wanaosimamia utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania kutekeleza mradi huo bila kujali itikadi za dini wala siasa kwani suala la maendeleo kwa wananchi halina ubaguzi.

Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo wakati akizindua kikao kazi cha utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania kilichofanyika leo jijini Arusha.

Mhe. Mchengerwa amesema, utekelezaji wa mradi huo utaendeleza na kuimarisha dhana ya uwazi, ukweli, ushirikishwaji na uwajibikaji kwani Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ina imani kuwa miradi ya kupunguza umaskini katika halmashauri zetu itaboresha maisha ya wananchi wengi na kuimarisha ustawi wao.

Amewakumbusha washiriki wa kikao kazi hicho kuwa, utekelezaji wa mradi huu unahitaji umakini mkubwa ili kuhakikisha miradi ya kijamii inayotekelezwa inaonyesha thamani ya fedha, hivyo amewataka wajumbe wazingatie maelekezo ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mhe. Mchengerwa amewasisitiza Viongozi na Watendaji kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia miongozo iliyowekwa ili kumuunga mkono Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amesimama kidete kuhakikisha wananchi hususani wanyonge wanapata huduma bora za kijamii ili kupunguza umaskini.

Akizungumzia juu ya matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, Mhe. Mchengerwa amemtaka Mkurugenzi Mtandaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuishirikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika kila mkoa ili kujiridhisha na uwepo wa tija ya miradi hiyo kwa wananchi na ni kwa namna gani miradi hiyo itaweza kuwakomboa.

“Mimi kama Waziri wa Utawala Bora, sitarajii kusikia ubadhirifu wa aina yoyote katika mikoa yote hiyo mitano ambayo miradi hii imeilenga, na pia sitegemei kusikia TAKUKURU inakwenda kupambana badala ya kwenda kuzuia ili tuweze kupata tija tuliyokusudia,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amesema, ni jukumu la kila mmoja katika mkoa na wilaya kufanya ufuatiliaji wa karibu na kwa umakini mkubwa wa matumizi ya fedha ya kila mradi kwani utekelezaji wa miradi hiyo ndio kipimo cha kila kiongozi na mtendaji kwenye ngazi ya mikoa na wilaya.

“Ni jukumu la kila Kiongozi, Watendaji, Maafisa wote wa Halmashauri zote, Waratibu wa TASAF na Maafisa wa TAKUKURU katika kila mkoa na wilaya kusimamia fedha za miradi zinazotolewa na Mhe. Rais kwa lengo la kuzinyanyua kaya zilizo na hali ngumu na kuondosha mazingira duni katika maeneo yao kwani hicho ndio kipimo chenu cha utendaji,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Akimkaribisha Mhe. Mchengerwa kuzindua Mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha. Mhe. John Mongella amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kufanya uzinduzi katika Mkoa wa Arusha na kuahidi kufanyia kazi maelekezo ambayo Mhe. Mchengerwa amekuwa akiyatoa sehemu mbalimbali juu ya usimamizi mzuri wa miradi inayotekelezwa na Serikali.

Amesema Mhe. Samia amekuwa akifanya mambo makubwa kwani amekuwa akitoa fedha nyingi hivyo, hawana budi kumuunga mkono na kuahidi kuwa hakuna ubadhirifu wowote utakaotokea katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga ameleezea lengo la kikao kazi hicho kuwa ni kuelekezana juu ya majukumu ya kila mmoja atakayeshiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Lengo la utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania ni kuwakomboa wananchi dhidi ya mazingira ya umaskini, maradhi na ujinga kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za kiuchumi, kijamii katika ngazi zote za jamii zilizo katika halmashauri.

Miradi itakayotekelezwa katika awamu hiyo ni ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa, mabweni, zahanati, vituo vya afya nyumba za watumishi wa vituo vya afya na walimu, ujenzi na ukarabati wa vivuko, barabara za vijijini na vyanzo vya maji. Jumla ya miradi 1,500 itakatekelezwa katika wilaya 33 za Mikoa ya Arusha, Njombe, Simiyu, Geita na Mwanza.
Share To:

Post A Comment: