Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati) akizungumza na watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo cha Uhasibu Arusha kuhusu masuala ya kiutumishi wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Arusha yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili Watumishi hao.

Mtumishi wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Bi. Anna Nyambo akiwasilisha changamoto yake ya kiutumishi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo yenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Chuo cha Uhasibu Arusha.


Baadhi ya Watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (aliyekaa katikati meza kuu) wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo, iliyolenga kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili watumishi wa chuo hicho.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati mstali wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha mara baada ya kuzungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Arusha iliyokuwa na lengo la kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa chuo hicho. Kulia kwake ni Mkuu wa Chuo hicho cha Ufundi Arusha, Dkt. Musa Chacha.


Afisa Utumishi wa Ofisi ya Rais - UTUMISHI, Bi. Salama Mohamed (aliyenyoosha mkono) akifafanua jambo kwa baadhi ya Watumishi wa Chuo cha Uhasibu Arusha waliowasilisha changamoto za masuala ya kiutumishi wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) iliyolenga kutatua changamoto za watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo cha Uhasibu Arusha. Kushoto kwake ni Afisa Utumishi, wa Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Bw. Ally Ngowo.


Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha, Dkt. Musa Chacha (aliyenyoosha kidole) akimuonyesha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (aliyevaa kofia nyekundu) mchoro wa jengo la kituo cha afya katika Chuo cha Ufundi Arusha.

***************************

Na. Veronica Mwafisi­­-ARUSHA

Tarehe 16 Oktoba, 2021

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka Waajiri katika Taasisi za Umma kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwapatia haki kwa wakati Watumishi wa Umma wanaotekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuwajengea morali ya utendaji kazi.

Dkt. Ndumbaro ametoa wito huo jijini Arusha kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) akiwa kwenye ziara yake ya kikazi, yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili Watumishi hao wa umma.

Dkt. Ndumbaro amesema, suala la uzingatiaji wa haki za Watumishi wa Umma limepewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo viongozi katika Taasisi za Umma wanapaswa kutenda haki kwa watumishi walio chini yao ili watumishi hao waweze kufanya kazi kwa moyo na uzalendo.

Sanjari na hilo, Dkt. Ndumbaro amehimiza suala la uadilifu katika Utumishi wa Umma ambalo limepewa msisitizo na Serikali ya Awamu ya Sita hivyo amewataka viongozi katika taasisi zote za umma kuwa mfano wa kuigwa kwa uadilifu.

“Watumishi wa Umma tunapaswa kuwa waadilifu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo katika Utumishi wa Umma,” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.

Aidha, Dkt. Ndumbaro amehimiza uwajibikaji katika Utumishi wa Umma kwa kuwataka viongozi na Watumishi wa Umma kuwajibika ipasavyo kwa Serikali iliyopo madarakani kwa wananchi wanaofuata huduma katika Taasisi za Umma.

“Serikali inawahimiza waajiri kuhakikisha Watumishi wa Umma wanafanya kazi kwa bidii, juhudi, maarifa na watambue mchango wa watumishi wanaofanya kazi kwa bidii,” Dkt. Ndumbaro amefafanua.

Kuhusiana na watumishi wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao, Dkt. Ndumbaro amewataka waajiri kuwachukulia hatua stahiki ili wabadilike na kuendana na Kaulimbiu ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya KAZI IENDELEE.

“Tuwachukulie hatua watumishi wote wanaobainika kutofanya kazi kwa bidii, tuwarekebishe kwa maneno au kuwaandikia barua, hivyo wasionewe haya kwani wataharibu taswira nzuri ya Utumishi wa Umma,” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku moja jijini Arusha, iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua kero na changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: