Serikali  imetoa Shilingi bilioni 97  kwa ajili ya kupambana na maambukizi ya TB ikiwemo kuimarisha huduma za afya vijijini na kupata takwimu sahihi.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri Dkt.Godwin Mollel wakati wa uzinduzi wa Muungano wa wadau wa kupambana na kifua kikuu Tanzania ulioshirikisha wabunge, viongozi wa dini taasisi na zingine.

Dkt. Mollel amesema Wizara inatarajia kuwafikia watu wengi kwa kutumia magari ambayo ni Mobile kliniki jambo ambalo linakwenda kumaliza changamoto ya ugonjwa huo na kupeleka elimu ya moja kwa moja kwa jamii ya chini akisema lengo la kutokomeza TB ifikapo 2030 wanaamini kuwa litafikiwa.

Aidha, Dkt.Mollel amezungumzia Muswada wa Bima ya afya kwa wote sasa umeiva kwani hivi karibuni ulitoka mikononi mwa kamati ya Makatibu Wakuu na sasa unapelekwa baraza la Mawaziri ili waupitie na kuuwasilisha bungeni Novemba mwaka huu.

Naye,Dkt.Saitole Laizer aliyemuwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali amesema ugonjwa huo bado ni tishio nchini ingawa watu wengi hawajui kuwa unaua na utaendelea kuua ikiwa juhudi za makusudi hazitachukuliwa kwa haraka.

"Vipimo vinaonyesha kati ya watu 133,000 wanaofikiwa kwa ajili ya vipimo vya TB, 227 hukutwa na maambukizi ya ugonjwa huo ambao kwa sasa Tanzania ina jumla ya wagonjwa wenye TB sugu 1600 nchini kote, 400 wakigundulika mwaka jana pekee". Amesema Dkt. Saitore

Hata hivyo ametaja changamoto ni kutokuwafikia baadhi ya makundi yenye uhatarishi wa ugonjwa ikiwemo watumiaji wa dawa za kulevya na wanaojidunga sindano aliosema ni miongoni mwa makundi hatari zaidi.

“Serikali imetupatia fedha nyingi ambazo zimefanikisha kununua magari mapya matano yatakayofanya kazi hadi vijijini kwa ajili ya vipimo vya kwa watu wanaoshindwa kufika hospitalini, hivyo mapambana haya yanatakiwa kuwa endelevu kwa nguvu na kwa kila mmoja wetu,” amesema Dkt. Saitore.

Akizindua muungano huo Spika wa bunge Job Ndugai amesema kuwa TB ni miongoni mwa magonjwa yanayoua kwa wingi Tanzania na duniani ambayo hayatakiwi kufanyiwa mchezo katika mapambano yake.

Spika Ndugai amewataka Watanznaia kujihadharisha na kuchukua hatua wanapoona kuna dalili kwani ugonjwa unaweza kumpata mtu yeyote na wakati wowote lakini akaomba taasisi ziwekeze fedha kwa vyombo vya habari ili elimu ya ugonjwa huo ipelekwe hadi maeneo ya vijijini.


Share To:

Post A Comment: